Kimataifa

New Zealand kutathmini upya sheria za umiliki wa bunduki

March 19th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

WELLINGTON, New Zealand

WAZIRI Mkuu wa New Zealand, Jacinda Arden, amesema taifa lake limeanza kutathmini upya sheria ya umiliki wa bunduki.

Hii ni kufuatia shambulio katika misikiti miwili mjini Christchurch wiki iliyopita, ambapo watu 50 waliuawa.

“Tumefanya uamuzi mkali kwenye mkutano wa baraza la mawaziri, ambapo sheria hiyo itaangaliwa tena. Hatutatishika hata kidogo. Lazima tuhakikishe kuwa maisha ya watu wetu yanalindwa kwa vyovyote vile,” akasema Arden.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa serikali imeanza uchunguzi kuhusu shambulio hilo.

“Lazima tutathmini sheria hii, ili kuhakikisha kwamba wale wanaomiliki bunduki ni watu wanaotambulika kwa urahisi, na habari zinazowahusu kuwekwa katika hifadhi maalumu,” akasema.

Shambulio hilo limesababisha hofu kutanda katika taifa hilo lenye utulivu mkubwa.