Newcastle pua na mdomo kuingia fainali ya Carabao Cup baada ya kukomoa Southampton katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali

Newcastle pua na mdomo kuingia fainali ya Carabao Cup baada ya kukomoa Southampton katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali

Na MASHIRIKA

NEWCASTLE United walinusia rekodi ya kuwahi kutinga fainali ya Carabao Cup kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kupokeza Southampton kichapo cha 1-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya kipute hicho mnamo Jumanne usiku ugani St Mary’s.

Bao la pekee na la ushindi katika pambano hilo lilifumwa wavuni na nyota wa Brazil, Joelinton de Lira, baada ya kukamilisha krosi aliyomegewa na Alexander Isak kunako dakika ya 73.

Iwapo watajikatia tiketi ya fainali ambayo itawakutanisha na Manchester United au Nottingham Forest, basi Newcastle ya kocha Eddie Howe itakuwa imeweka historia ya kunogesha fainali ya kombe la haiba kubwa kwa mara ya kwanza tangu 1999 walipofuzu kwa fainali ya Kombe la FA.

Ushindi dhidi ya Southampton uwanjani St Mary’s mnamo Jumanne usiku pia uliweka hai ndoto ya Newcastle kunyanyua taji la kwanza tangu watawazwe wafalme wa kipute cha Inter-Cities Fairs Cup mnamo 1969.

Wanapojiandaa kwa marudiano ya nusu-fainali ugani St James’ Park siku sita zijazo, Newcastle watapania kuchuma nafuu ya kuchezea nyumbani kumtegemea pakubwa kipa Nick Pope aliyewajibishwa vilivyo na Che Adams katika mkondo wa kwanza.

Ingawa Adams alifungia Southampton mnamo Jumanne, goli lake lilifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR, tukio lililomkera beki Duje Caleta-Car aliyeishia kulishwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu.

Awali, bao la Joelinton nalo lilikataliwa mapema na refa kwa madai kuwa alicheka na nyavu za wageni wao akiwa ameotea. Newcastle pia ni miongoni mwa timu zinazowania fursa ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora msimu huu na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Kufikia sasa, wanakamata nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 39 sawa na wafalme mara 20 wa EPL, Manchester United. Arsenal wanaselelea kileleni mwa pointi 50, tano zaidi kuliko nambari Manchester City ambao ni mabingwa watetezi.

Newcastle walijitosa ugani Jumanne wakipigiwa upatu wa kutandika Southampton ikizingatiwa kuwa ni Man City pekee ndio walikuwa wameondoka ugani St Mary’s bila kufunga bao kutokana na mechi 15 zilizopita ambazo zimetandazwa na The Saints nyumbani.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu 1975-76 kwa Newcastle kunogesha nusu-fainali ya Carabao Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Mwenye kilabu alikofia mbunge wa zamani George Thuo kuanza...

Maneno ya mwisho ya Magoha kwa Machogu akichukua usukani

T L