Newcastle United na mbwa-mwitu Wolves nguvu sawa kwenye gozi la EPL

Newcastle United na mbwa-mwitu Wolves nguvu sawa kwenye gozi la EPL

Na MASHIRIKA

NAHODHA Jamaal Lascelles wa Newcastle United amewataka wanasoka wenzake katika kikosi hicho kujituma maradufu ili kujitoa katika hatari ya kuwa miongoni mwa vikosi vinavyochungulia hatari ya kuteremshwa daraja mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Newcastle dhidi ya Wolves mnamo Jumamosi uwanjani St James’ Park iliwasaza katika nafasi ya 17 kwa alama 26 sawa na Brighton waliopigwa 1-0 na West Bromwich Albion ugani The Hawthorns.

Ni pengo la alama nne pekee ndilo linatenganisha Newcastle na Fulham ambao kwa pamoja na West Brom na Sheffield United, wanakamata nafasi tatu za mwisho kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Pigo zaidi kwa Newcastle mwishoni mwa mchuano wao na Wolves ni jeraha ambalo kocha Steve Bruce sasa amethibitisha kwamba litamweka nje fowadi raia wa Paraguay, Miguel Almiron kwa kipindi kirefu kijacho.

Almiron aliondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili, dakika chache kabla ya Newcastle kuweka kifua mbele na Lascelles aliyejaza kimiani krosi ya Ryan Fraser.

Hata hivyo, juhudi za Lascelles zilifutwa na fowadi Ruben Neves aliyesawazishia waajiri wake kunako dakika ya 73 na kuwavunia Wolves alama moja iliyowadumisha katika nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 34 sawa na Arsenal ya kocha Mikel Arteta.

Neves alishirikiana pakubwa na Pedro Neto na Martin Dubravka aliyewajibishwa na kocha Nuno Espirito kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wazima kambini mwa Wolves.

Wolves kwa sasa wanajiandaa kuwa wageni wa Man-City mnamo Machi 2, 2021 kabla ya kuchuana na Aston Villa mnamo Machi 6, siku moja kabla ya Newcastle kuwaendea West Brom ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa biriani ya nyama ya mbuzi

JAMVI: Kusambaratika kwa NASA huenda itakuwa nafuu au...