Newcastle United na West Ham nguvu sawa katika EPL ugani St James’ Park

Newcastle United na West Ham nguvu sawa katika EPL ugani St James’ Park

Na MASHIRIKA

WEST Ham United walitoka nyuma na kulazimishia Newcastle United sare ya 1-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani St James’ Park.

Sean Longstaff aliyefunga mabao mawili dhidi ya Southampton mnamo Januari 31, 2023 na kusaidia Newcastle kufuzu kwa fainali ya Carabao Cup alishirikiana vilivyo na Callum Wilson aliyeweka waajiri wake kifua mbele katika dakika ya tatu.

Fabian Schar nusura afanye mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 10 kabla ya West Ham kusawazishiwa na Lucas Paqueta kunako dakika ya 32. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Newcastle kufungwa ligini tangu Novemba 6, 2022. Kikosi hicho cha kocha Eddie Howe sasa kimeambulia sare mara nne kutokana na mechi tano zilizopita za EPL.

Licha ya kujituma vilivyo katika vipindi vyote viwili vya mchezo, Newcastle walikosa kufunga bao la ushindi katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa fowadi Allan Saint-Maximin kunogesha ligini tangu Agosti 28, 2022.

Matokeo hayo yaliteremsha Newcastle hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 40, mbili nyuma ya nambari tatu Manchester United waliokomoa Crystal Palace 2-1 ugani Old Trafford licha ya kiungo mkabaji Carlos Casemiro kuonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili.

Ni pengo la alama nne ndilo linatamalaki kati ya Newcastle na nambari tano Tottenham Hotspur watakaokuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Manchester City mnamo Februari 5, 2023. Man-City wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 45 huku West Ham wakisalia katika nafasi ya 16 kwa pointi 19 baada ya mechi 21.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Everton 1-0 Arsenal

Aston Villa 2-4 Leicester

Brentford 3-0 Southampton

Brighton 1-0 Bournemouth

Man-United 2-1 Crystal Palace

Wolves 3-0 Liverpool

Newcastle 1-1 West Ham

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Manchester United wazamisha Palace katika EPL ugani Old...

Lionel Messi abeba PSG dhidi ya Toulouse katika Ligi Kuu ya...

T L