Newcastle washauriwa kumpuuza Pochettino na kumpa Benitez mikoba yao ya ukocha

Newcastle washauriwa kumpuuza Pochettino na kumpa Benitez mikoba yao ya ukocha

Na CHRIS ADUNGO

NEWCASTLE United wameshauriwa kutompa kocha Mauricio Pochettino mikoba yao ya ukocha kwa sababu “hajawahi kushinda chochote” katika taaluma yake ya ukufunzi.

Newcastle United wapo katika hatua za mwisho za kununuliwa na mabwanyenye wa Saudi Arabia kwa kima cha Sh420 bilioni.

Kukamilika kwa mchakato huo kunatarajiwa kushuhudia wamiliki wapya wa Newcastle wakimfurusha kocha Steve Bruce na kujitosa sokoni kumsaka mkufunzi mpya huku Pochettino na Rafa Benitez wakihusishwa pakubwa na mikoba ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mvamizi wa zamani wa Newcastle, Michael Chopra anaamini kwamba itakuwa vyema zaidi kwa timu hiyo kumpokeza Benitez ambaye ni mzawa wa Uhispania mikoba yao badala ya Pochettino ambaye ni raia wa Argentina.

“Kwa kweli Pochettino aliijenga Tottenham Hotspur, akawaongoza kujenga uwanja mpya, akawasaidia kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kwa wakati fulani akawaleta karibu sana na kushinda taji la EPL,” akatanguliza Chopra ambaye ni mzawa wa mji wa Newcastle, Uingereza

“Ingawa hivyo, hakuna taji lolote ambalo amewahi kutia kibindoni katika historia yake ya ukufunzi. Hilo linamweka mbele Benitez mbali na kuwa na sifa ya kuhusiana vyema na wachezaji na mashabiki, ana uwezo wa kunyanyua mataji iwapo atapokezwa fedha kiasi za kukisuka upya kikosi,” akaongeza.

“Benitez anajivunia historia pana ya ufanisi katika ulingo wa soka. Ana tajriba ya kuwakuza wachezaji chipukizi na kuwafanya masupastaa wa haiba kubwa. Amewahi kuwaongoza Liverpool, Chelsea na Napoli kunyanyua mataji wakati wa ukocha wake kambini mwa vikosi hivyo,” akasema Chopra ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa kikosi cha Dalian Pro cha Ligi Kuu ya China.

You can share this post!

Kocha Pasuwa wa Big Bullets ya Malawi akataa ofa ya kuinoa...

Kahata arejea kambini mwa Simba SC huku ligi kuu ya TZ...

adminleo