Michezo

Neymar afunga mawili na kusaidia PSG kuponda Angers 6-1

October 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MFUMAJI Neymar Jr alifunga mabao mawili na kuwaongoza waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kuwapepeta Angers 6-1 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na hivyo kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi Rennes hadi pointi moja pekee.

Neymar alipachika wavuni mabao yake kunako dakika za 36 na 47 baada ya Alessandro Florenzi kuwafungulia PSG ukurasa wa mabao katika dakika ya saba.

Ingawa Ismael Traore alipania kuwarejesha Angers mchezoni, PSG walifanya mambo kuwa 4-1 kupitia Julian Draxler katika dakika ya 57 kabla ya magoli ya Idrissa Gueye na Kylian Mbappe mwishoni mwa kipindi cha pili kuzamisha kabisa chombo cha Angers waliokuwa ugenini.

Ushindi huo ulikuwa wa nne mfululizo kwa PSG kusajili msimu huu baada ya kupoteza michuano miwili ya ufunguzi wa msimu huu wa 2020-21.

Mabao ya Neymar yalikuwa yake ya kwanza msimu huu tangu arejee ugani baada ya kutumikia marufuku ya mechi mbili kwa kuzua fujo katika mechi iliyoshuhudia PSG wakipigwa 1-0 na Marseille mnamo Septemba 13, 2020.

Fowadi raia wa Argentina, Angel Di Maria, aliyekuwa kati ya wanasoka watano walioadhibiwa vikali kwa kuhusika katika fujo hizo, bado ana mechi mbili za kuwa nje baada ya kupigwa marufuku ya michauno minne.

Rennes ambao wanadhibiti kilele cha jedwali la Ligue 1, hawajapoteza mechi yoyote kati ya tano zilizopita, na watakuwa wenyeji wa Reims wanaokokota nanga mkiani mnamo Oktoba 4, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO