Michezo

Neymar akosa mazoezi PSG, tetesi za kurejea Barcelona zikishika kasi

July 9th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

MABINGWA wa Ligue 1 Paris Saint Germain (PSG) wametangaza kwamba watamchukulia hatua kali nyota wao Neymar Jr kwa kukosa kufika uwanjani katika siku ya kwanza ya mazoezi kambini mwa timu hiyo inayojifua kwa msimu mpya wa 2018/19.

Neymar alitarajiwa kujiunga na wenzake mazoezini mnano Jumatatu Julai 8, 2019, lakini akakosa kufika huku tetesi zinazomhusisha na kurejea Uhispania kuwajibikia Barcelona zikizidi kushika kasi.

“PSG inatambua kwamba Neymar hakufika mazoezini na hakupata ruhusa kutoka kwa klabu. Klabu inasikitikia hali hii,” ikasema habari kutoka PSG.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa PSG Leonardo Araujo awali alinukuliwa na jarida moja la nchini Ufaransa akisema kwamba klabu hiyo itasalia tu na wachezaji wenye nia ya kuiwajibikia lakini akafichua kwamba Barcelona haijawasilisha rasmi ofa ya kutaka kutwaa huduma za nyota wao wa zamani.

“Neymar anaweza kuondoka PSG kama kuna ofa inayoridhisha pande zote. Hadi sasa hatujui kama kuna klabu yeyote inayotaka kumnunua na kwa bei gani. PSG itategemea wachezaji wanaofurahia kuisakati ili izidi kujenga himaya kama klabu bora ya soka duniani,” akasema Leonardo.

Vyombo vya habari nchini Brazil zilimnukuu babake mchezaji huyo, Neymar Sr akisema PSG walikuwa na habari kwamba mwanawe angekosa mazoezi hayo kutokana na kukabwa na majukumu ya kuwasaidia wasiojiweza katika jamii kupitia taasisi yake.

“Sababu ya kukosa mazoezi ilijulikana kwa kuwa alikuwa amepanga shughuli za taasisi yake mapema. Hatungeweza kuahirisha shughuli hizi. Atarejea PSG Julai 15,” akaeleza jarida la spoti nchini humo kwa jina Fox.

Neymar alijiunga na PSG kutoka Barcelona Agosti 2017.

Licha ya kukabiliwa na matukio kadhaa ya ukosefu wa nidhamu uwanjani msimu uliokamilika wa 2018/19, alifungia timu hiyo mabao 34 katika mechi 37 na kuisadia kutwaa ubingwa wa Ligue 1.

Vilevile alipigwa marufuku kushiriki mechi tatu za ligi kwa kutishia kumtandika shabiki baada ya kushindwa kwenye mechi ya Kombe la Ufaransa na Rennes na pia atakosa mechi tatu za Klabu Bingwa Barani Ulaya kwa kuwafokea wasimamizi wa mechi.