Michezo

Neymar apinga tetesi alimbaka mwanamke

June 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

MWANASOKA mahiri Neymar wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) amekanusha madai ya kumbaka mwanamke jijini hapa.

Kulingana na ripoti ya polisi, mwanammke huyo amedai kwamba tukio hilo lilifanyika katika hoteli moja jijini hapa.

Akijitetea, Neymar amewasilisha ujumbe wa kurekodiwa unaoonyesha kila alichokiita mflulizo wa ujumbe wa Whatsapp kati yake na mwanamke huyo.

Kwa sasa mwanasoka huyo yuko nchini Brazil na timu ya taifa kujiandaa kwa michuano ya Copa America itakayofanyika nchini Brazil kati ya Juni 14 na Julai 7 ambapo timu yake itacheza dhidi ya Bolivia, Venezuela na Peru katika mechi za Kundi A.

Kulingana na uchunguzi wa polisi, mwanamke huyo ambaye jina lake halikutajwa alijuana na Neymar kupitia mtandaoni ndipo wakakubaliana wakutane jijini Paris ana kwa ana, lakini sasa ameanza kudai kwamba Neymar alimfanyia kitendo hicho na akatoka akiwa mlevi.

Mwanamke huyo amedai mwanasoka huyo alimtumia tiketi ya ndege kutoka Brazil kuelekea Ufaransa mwezi Mei na kumlipia chumba cha kulala katika hoteli ya kifahari ya Sofitel Paris arc Du Triomp.

“Baada ya mazungumzo, Neymar alimkumbatiana naye, hadi ikafikia kiwango cha Neymar kuanza kumlazimisha wafanye mapenzi, hapo ndipo alipojamiiana na mwanamke huyo bila idhini yake,” taarifa ya polisi ilisema.

Mwanamke huyo alirejea Brazil siku mbili baadaye, bila kuripoti tukio hilo kwa polisi nchini Ufaransa, kwa kuwa alikuwa amejawa na hofu kuwasilisha malalamishi yake katika taifa geni, taarifa hiyo iliendelea.

Lakini mwanasoka huyo amepuuzilia mbali madai hayo akidai hayana msingi wala chembe ya haki, huku akisisitiza kwamba mwanamke huyo ameshirikiana na maadui zake kumharibia jina kwa lengo la kumla pesa.

Kwa kuthibitisha madai yake, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amechapisha video yake ya kujitetea na kujitenga na tuhuma hizo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.

“Kutokana na kulazimishwa kutoa fedha, ninalazimika kuanika maisha yangu na ya familia yangu wazi,” alisema.

“Kilichotokea siku ile kilikuwa cha faragha ya wapenzi wawili, yalikuwa ni mahusiano ya mwanaume na mwanamke ndani ya kuta nne. Siku ya pili hakukuwa na mengi yaliyotokea. Tuliendelea kutumiana ujumbe kwenye simu, akaniomba nimtumie zawadi (ya mtoto wake),” akadai Neymar.

Ujumbe wa simu

Kwenye video, Neymar ameonyesha msururu wa kile alichokiita ujumbe wa simu baina yake na mwanamke huyo pamoja na picha za msichana huyo akiwa amevalia nguo zake za ndani tu.

Babake Neymar, Dos Santos pia aliwaambia waandishi kwamba mwanawe alikuwa amewekewa mtego.

“Iwapo umma hautaambiwa ukweli kuhusu kisa hiki na iwapo hatuwezi kuonyesha ukweli kwa haraka, tuhuma hizo zitakuwa kubwa. Iwapo tutalazimika kuonyesha mawasiliano ya Neymar ya Whatsapp na msichana huyo tutayaonyesha,” aliongeza Dos Santos.

Kufikia sasa, Neymar amepokonywa unahodha wa timu ya Brazil kutokana na madai ya utovu wa nidhamu kwa kumshambulia shabiki baada ya PSG kushindwa na Rennes katika pambano Kombe la Ufaransa yaani Coupe De France mwezi uliopita.