Michezo

Neymar nje mechi mbili kwa utovu wa nidhamu

September 18th, 2020 2 min read

NA MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa:

Supastaa Neymar amepigwa marufuku michuano miwili kwa kupiga kofi mchezaji wa Marseille Alvaro Gonzalez.

Hata hivyo, Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) imethibitisha inachunguza madai ya mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain kuwa alibaguliwa kwa misingi ya rangi.

Mbrazil huyo, ambaye alikodolea macho marufuku ya mechi saba kwa kosa hilo, hakuwa uwanjani timu yake ya PSG ikiandikisha ushindi wake wa kwanza kwa kuzaba Metz 1-0 hapo Septemba 16.

Neymar alikuwa katika orodha ya wachezaji watano waliolishwa kadi nyekundu ghasia za kushangaza zilipozuka katika dakika za lala-salama PSG ikipoteza 1-0 dhidi ya Marseille mnamo Septemba 13.

Tovuti ya Get French Football News inadai kuwa wachezaji wote watano waliohusika katika mapigano hayo watatumikia marufuku.

Kamati ya nidhamu ya Ligue 1, inayokutana kila Jumatano, iliamua kupiga beki wa PSG Layvin Kurzawa na kiungo Leandro Paredes marufuku ya mechi sita kila mmoja.

Mshambuliaji wa Marseille Dario Benedetto atakosa mchuano mmoja naye mchezaji mwenza Jordan Amavi atakuwa nje mechi tatu zijazo.

Neymar, ambaye ni mchezaji ghali wa PSG, alionyeshwa kadi nyekundu teknolojia ya VAR ilipothibitisha kuwa alirushia Gonzalez konde kisogoni, lakini Mbrazil huyo ameshutumu Mhispania huyo kwa kumtusi.

Katika taarifa ndefu kwenye mtandao wake wa Twitter, Gonzalez alijitetea, “Ubaguzi hauna nafasi katika maeneo yetu”.

Hata hivyo, serikali ya Brazil na klabu ya PSG zinasimama na Neymar kufuatia madai hayo, na sasa Ligue 1 inachunguza kesi hiyo.

Neymar alichukua sheria mikononi mwake akidai baadaye kwenye Twitter kuwa Gonzalez si ‘mwanamume’, ni mtu anayeamini kuwa jamii yake ni bora kuliko nyingine’ na anadai kuwa hakuheshimu mpinzani wake.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 28 aliongeza taarifa yake kwenye Instagram akieleza kuwa “alichukizwa” na “hangekataa kitako bila ya kuchukua hatua”.

Marseille ilitoa taarifa Jumatatu ikipuuzilia mbali madai ya Neymar kuhusu Gonzalez. Beki huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye ripoti nchini Ufaransa zinadai anakabiliwa na marufuku ya mechi 10, amepokea vitisho dhidi ya maisha yake.

Taarifa ya Marseille ilisema, “Alvaro Gonzalez si mtu anayebagua, ametuonyesha hivyo kupitia tabia yake ya kila siku tangu ajiunge na klabu hii, na wachezaji wenzake tayari wametoa ushahidi.”

Inaaminika pia nyota wa PSG Angel Di Maria anatarajiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Ligue 1 kufuatia madai kuwa alitema mate alikokuwa Gonzalez.

Idadi ya kadi nyekundu katika kambi ya PSG ziliongezeka hapo Jumatano pale beki Abdou Diallo alipopokea kadi ya njano katika kila kipindi kwa kucheza visivyo dhidi ya Metz.

TAFSISI: GEOFFREY ANENE