Michezo

Neymar wa PSG aondolewa uwanjani kwa machela baada ya kupata jeraha baya dhidi ya Lyon waliowapiga 1-0 ligini

December 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI Neymar Jr wa Paris Saint-Germain (PSG) aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kupata jeraha baya la kifundo cha mguu katika mchuano wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) uliowakutanisha na Olympique Lyon mnamo Disemba 13, 2020.

Lyon walisajili ushindi wa 1-0 katika mchuano huo uliochezewa uwanjani Parc des Princes.

Neymar ambaye ni raia wa Brazil alionekana akipiga akijigaragaza uwanjani kwa maumivu makali mwishoni mwa mechi huku akishika kifundo cha mguu baada ya kuchezewa visivyo na Thiago Mendes aliyeonyeshwa kadi nyekundu.

Tino Kadewere ndiye aliyefungia Lyon bao la pekee na la ushindi dhidi ya PSG walioshuka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 kwa alama 28, moja nyuma ya viongozi Lille na Lyon.

Kocha Thomas Tuchel amesema wanasubiri tathmini ya madaktari wa PSG ili kubaini urefu wa muda ambao Neymar atahitaji mkekani kabla ya kupona.

Neymar, 28, alijiunga na PSG mnamo Agosti 2017 baada ya kuagana na Barcelona ya Uhispania kwa Sh26 bilioni – fedha zilizomfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani.

Tangu wakati huo, amewasaidia PSG kutwaa ubingwa wa Ligue 1 mara tatu mfululizo na kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara moja.