Habari za Kitaifa

NG-CDF yamulikwa kwa wasimamizi kuwa na vyeti ghushi

March 7th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inachunguza madai kwamba baadhi ya mameneja wanaohudumu katika Bodi ya Kitaifa ya Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) waliajiriwa baada ya wao kuwasilisha stakabadhi ghushi.

Tume hiyo Jumatano ilisema kuwa imepata ripoti kwamba baadhi ya maafisa wakuu walioajiriwa na bodi ya NG-CDF wana stakabadhi ghushi za masomo.

EACC pia ilisema kuwa inachunguza madai kuwa bodi ya NG-CDF ilifeli kuchukua hatua zozote dhidi ya wafanyakazi wake wanaodaiwa kuwa na stakabadhi feki baada ya kujulishwa kuhusu suala hilo.

Katika kisa kimoja, EACC ilisema kuwa chuo kimoja kikuu nchini kiliandikia bodi hiyo barua kikiiambia kuwa cheti kimoja cha shahada ya digrii ambacho meneja mmoja aliwasilisha kwa afisi zake akisaka ajira, kilikuwa ghushi.

“Tunachukulia suala hilo kwa uzito na tutatoa mwelekeo baada ya kukamilisha uchunguzi wetu,” afisa mmoja wa cheo cha juu katika EACC alisema.

Inadaiwa kuwa meneja huyo aliwasilisha cheti cha Digrii ya Kwanza katika Usimamizi wa Biashara ambacho inadaiwa kuwa ni ghushi.

Chuo hicho kilikataa kuthibitisha uhalali wa cheti hicho na kujulisha Bodi ya Kitaifa ya NG-CDF kuhusu suala hilo.

EACC iliahidi kushughulikia suala hilo na kukomboa pesa zote ambazo watu wenye stakabadhi ghushi walitumia kuwawezesha kupata ajira katika asasi zote za serikali kuu na zile za kaunti.

Majuma matatu yaliyopita, mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) Anthony Muchiri alisema uchunguzi wao umebaini kuwa jumla ya watumishi 2,064 walipata ajira na walipandishwa vyeo kwa kutumia stakabadhi ghushi za masomo na taaluma.

Swali ni je, maafisa wa vyeti feki wanaweza wakatekeleza uadilifu kwa kupeana basari kuwezesha wanafunzi kuendelea na masomo?