Michezo

NGANGARI: Stars yaweka wazi mikakati ya Afcon Migne akitaja vifaa

May 15th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sebastien Migne wa Harambee Stars atapania kutegemea huduma za wachezaji wengi wanaosakata soka ya kulipwa katika mataifa ya kigeni kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri mwaka huu.

Jumanne, mkufunzi huyo mzawa wa Ufaransa alikitaja kikosi cha wanasoka 26 ambao anawatarajia kujinoa vilivyo kwa kampeni za AFCON zitakazoandaliwa Misri kati ya Juni 21 na Julai 19.

Winga matata wa AFC Leopards, Paul Were na John Avire wa Sofapaka ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaikamilisha orodha ya Migne iliyokosa tena jina la mshambuliaji Jesse Were wa Zesco United, Zambia.

Clifton Miheso ambaye kwa sasa anawasakatia Clube Olimpico do Montijo ya Ureno pia anaunga kikosi hicho ambacho kwa sasa kinatarajiwa kutua nchini Ufaransa kujifua kwa kipindi cha majuma matatu kabla ya kuelekea Misri kwa kipute cha AFCON 2019.

Wakiwa Ufaransa, Stars wamepangiwa kuchuana na Madagascar na Gambia katika mechi mbili za kujipa nguvu. Mfumaji Bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hadi kufikia sasa, Allan Wanga wa Kakamega Homeboyz ni miongoni mwa mafowadi saba ambao wanatarajiwa kuongoza safu ya mbele ya Stars ambao wanarejea kuwania ubingwa wa Kombe la Afcon baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka 15.

Kenya ilishiriki kampeni za Afcon kwa mara ya mwisho mnamo 2004 nchini Tunisia chini ya mkufunzi Jacob ‘Ghost’ Mulee.

Kenya wametiwa katika Kundi C pamoja na Senegal, Algeria, na majirani zao kutoka Afrika Mashariki, Tanzania.

Kikosi cha Migne kimeratibiwa kufungua kampeni za AFCON dhidi ya Algeria mnamo Juni 23 katika uwanja wa Cairo June 30 Stadium.
Stars ambao wanarejea kunogesha kivumbi cha AFCON baada ya kukosa uhondo wa makala saba yaliyopita.

Chini ya Migne, wachezaji 26 waliotajwa jana wanatarajiwa kuelekea Ufaransa mnamo Mei 31 kupiga kambi ya mazoezi kabla ya kupimana ubabe na Madagascar mnamo Juni 7 kisha Gambia hapo Juni 15 jijini Paris halafu kutua Misri mnamo Juni 19.

Baada ya kunyanyuana na Algeria katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi C, Stars wanaojivunia maarifa ya kiungo Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur nchini Uingereza, watachuana na Tanzania mnamo Juni 27 kisha Senegal hapo Julai 1.

Senegal wanaojivunia huduma za mvamizi Sadio Mane wa Liverpool watafanyia mazoezi yao nchini Uhispania. Miamba hao wa soka ya Afrika watapimana na Super Eagles ya Nigeria mnamo Juni 16.

Mikakati

Algeria anayochezea nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez, haijaanika mikakati yake.

Tanzania ya mkufunzi mzawa wa Nigeria Emmanuel Amuneke, ilifichua kikosi cha wachezaji 39 mnamo Mei 2. Timu hiyo itapimana nguvu na Misri mnamo Juni 13.

Kikosi cha Stars

MAKIPA: Patrick Matasi (St Georges, Ethiopia), Faruk Shikhalo (Bandari, Kenya), John Oyemba (Kariobangi Sharks, Kenya), Brian Bwire (Sharks).

MABEKI: Philemon Otieno (Gor Mahia, Kenya), Musa Mohammed (Nkana FC, Zambia), Joash Onyango (Gor Mahia), Aboud Omar (Sepsi Sfantu, Romania), David Owino (Zesco United, Zambia), Bernard Ochieng (Vihiga United, Kenya), Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), Erick Ouma (Vasalund IF, Uswidi), Joseph Okumu.

VIUNGO: Victor Wanyama (Tottenham Hotspur, Uingereza), Anthony Akumu (Zesco United), Eric Johanna (IF Bromma, Uswidi), Ismael Gonzales (UD Las Palmas, Uhispania), Francis Kahata (Gor Mahia), Dennis Odhiambo (Sofapaka, Kenya), Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Christopher Mbamba (Oskarshamns AIK, Uswidi), Whyvonne Isuza (AFC Leopards, Kenya), Clifton Miheso (Clube Olimpico, Ureno).

WAVAMIZI: Paul Were (AFC Leopards), Ayub Timbe (Beijing Renhe, China), Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz, Kenya), John Avire (Sofapaka), Masud Juma (Libya), Ochieng Ovella (IF Vasalund).