Michezo

Ngarambe ya Super 8 yaanza

September 23rd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

KINYANG’ANYIRO cha kufukuzia taji la Super Eight Premier League (S8PL) kinazidi kushusha upinzani wa kufa mtu msimu huu. Baadhi ya timu zinazoshiriki ngarambe hiyo zimejikuta zikiandisha matokeo mseto hali inayoendelea kubadilisha jedwali kinyume na matarajio ya wengine.

Katika mpango mzima mabingwa watetezi, Jericho Allstars imejipata kwenye wakati mgumu baada ya Githurai Allstars, Melta Kabiria na Mathare Flames kuendelea kutifua vumbi kali kwenye mechi za hivi karibuni.

Ingawa Githurai Allstars inayotiwa makali na kocha, Fredrick Onyango inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza hivi karibuni imeteleza mara kadhaa bado inazidi kutetesha wapinzani wao

kwenye kampeni za mwaka huu. Kasi ya kikosi hicho pia Melta Kabiria bila kuweka katika kaburi la sahau Mathare Flames imeitia Jericho Allstars presha zaidi kwenye harakati za kutetea taji hilo ililotwaa muhula uliyopita.

Wanasoka wa Team Umeme inayoshiriki kipute cha S8PL. Picha/ John Kimwere

”Matokeo ya hivi wiki mbili zilizopita yalivuruga mpango wetu kiasi kwenye kampeni za migarazano ya msimu huu,” alisema kocha huyo wa Githurai Allstars na kuongeza kuwa bado wanaamini wameketi pazuri kujibiidisha na kufanikiwa kufanya kweli.

Kadhalika anadokeza kuwa kamwe hawawezi kuyeyusha matumaini ya kubeba taji hilo msimu huu. Kocha wa Jericho Allstars mara kadhaa amenukuliwa akisema ”Licha ya upinzani mkali unaoshuhudiwa raundi hii tunalenga kuendelea kujituma kisabuni kufukuzia taji hilo.”

Githurai Allstars imeibuka ya kwanza kwenye mechi zote ambazo huandaliwa na Extreme Sports ambayo imekuwa ikishiriki kila ligi mara moja na kuibuka mabingwa.

Githurai ilishangaza wengi ilipobeba mataji matatu mfululizo na kufuzu kushiriki kipute hicho. Kwenye michuano ya kuwania taji la Super Eight Daraja la Kwanza, katika patashika ya mwisho kikosi hicho kilikomoa Huruma Kona mabao 2-1 na kumaliza kidedea kwa kufikisha alama 79.

Baadhi ya wachezaji wa NYSA wanaoshiriki kipute cha S8PL. Picha/ John Kimwere

Nayo NYSA iliyokuwa kati ya wapinzani wakuu kwenye kikwaruzano ya msimu uliyopita ianzidi kujikaza baada ya kuteleza kwenye katika kampeni za mkumbo wa kwanza.

NYSA ya kocha, Fredrick ‘Oti’ Otieno inashikilia nafasi ya nane kwa kukusanya 33, sawa na Team Umeme tofauti ikiwa idadi ya mabao. Wachana nyavu wa Team Umeme licha ya kutokuwa miongoni mwa nafasi tano bora kwenye msimamo wa michuano hiyo inaendelea kuvuruga matumaini ya timu nyingi mwaka huu.

Githurai Allstars ilipiga hatua ilipoandikisha ufanisi wa bao 1-0 dhidi ya Lebanon FC na kutwaa usukani wa kipute hicho kwa alama 43 sawa na Jericho Allstars tofauti ikiwa idadi ya mabao. Kwenye kampeni hizo, Githurai Allstars na Jericho Allstars zimecheza mechi 23 na 24 mtawalia.

Nayo Melta Kabiria iliyobamiza Huruma Kona kwa magoli 3-2 inashikilia tatu bora kwa kuzoa pointi 42, moja mbele ya wachezaji wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK).