Makala

NGARE: Rais apuuze mwito wa kubaki uongozini 2022

January 8th, 2020 2 min read

Na PETER NGARE

KILA kiongozi wa nchi huwa na watu wa karibu ambao humpa ushauri kuhusu masuala tofauti.

Katika baadhi ya mataifa, wandani wengi huwa vikaragosi vya kumsifu kiongozi kwa kumweleza tu yale mambo ambayo yatamfurahisha badala ya ukweli jinsi ulivyo.

Baradhuli hawa hutumia fursa hii ya kuwa karibu na rais fulani kupora mali ya umma na kuendeleza ajenda zao za kibinafsi bila kujali hali ya nchi.

Ni washauri hawa ambao mara nyingi humpotosha rais mhusika ili waweze kuendela kulinda maslahi yao, na mara nyingi wanakuwa hata tayari kutumbukiza taifa kwenye ghasia kwa ushauri mbaya wanaotoa kwa rais mhusika.

Mfano ni nchi ya Burundi ambayo miaka michache iliyopita ilikumbwa na maafa ya ghasia baada ya Rais Pierre Nkurunziza kukataa kuondoka madarakani kipindi chake kilipoisha.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda naye amekatalia madarakani kwa kubadilisha Katiba ili aendelee kutawala.

Aliyekuwa rais wa Sudan, Omar el-Bashir naye alikaa mamlakani kwa kubadilisha sheria ili kuendelea kushikilia uongozi wa nchi hiyo hadi alipoondolewa na raia mwaka 2019.

Hii ni mifano ya kusikitisha kuhusu viongozi wa Afrika waliojawa na ubinafsi, ulafi na kutojali mataifa yao.

Hawa ni viongozi baradhuli ambao wanakosa kuheshimu katiba za nchi zao walizoapa kulinda na badala yake wanabadilisha sheria na mifumo ili kuendelea kudhulumu wananchi.

Ni kwa misingi hii ambapo inasikitisha kusikia vikaragosi vya Rais Uhuru Kenyatta vikitangaza kuwa sheria itafanyiwa mabadiliko ili kumwezesha kuwa Waziri Mkuu 2022.

Rais Kenyatta anafaa kufahamu kuwa watu hawa anaodhani kuwa ni marafiki wake ni maadui ambao wanataka kumweka kwenye mtego wa kulaaniwa na vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuvuruga ustawi wa kidemokrasia hapa Kenya.

Kiongozi wa taifa anapasa kujua kuwa watu hawa wanaomwambia asiondoke madarakani wamejizolea mali na madaraka kwa kujihusisha naye, na sasa wamejaa wasiwasi kuhusu hali yao itakavyokuwa akiondoka.

Vikaragosi hivi vimejaa ubinafsi, ulafi na upofu ambao haujali maslahi ya wananchi na taifa hili wala Rais Kenyatta mwenyewe. mbali vinaangazia tu jinsi vitakavyoendelea kujaza matumbo kwa mali ya bwerere.

Kwa uhakika, utawala wako Rais Kenyatta umekumbwa na changamoto tele ambazo zimemuacha mwananchi wa kawaida katika umaskini zaidi, gharama ya maisha kupanda, madeni tele ya kigeni na mengine mengi.

Rais pia uliahidi kuwa katika muhula wako wa pili ungetimiza ajenda nne kuu, lakini hali ilivyo hii bado ni ndoto ya mchana.

Matatizo haya yamewaacha wananchi wengi wakiwa na machungu dhidi ya utawala wa Jubilee na hakuna uhakika kuwa wangetaka uongezewe muda wa kuwaongoza.

Wale ambao wanakudanganya kuwa ungali maarufu na ukiongezewa muda 2022 utaweza kutimiza ahadi zako wanakupotosha.

Hawa ni watu ambao wanataka uonekane kama kiongozi wa kidikteta anayekatalia madarakani, anayepuuza Katiba na asiyetegemeka kwani katika matamshi yako ya awali uliahidi kuwa utatawala kwa miaka 10 pekee.

Tafadhali Rais Kenyatta jua kuwa watu hawa wanaokupotosha ni nyani ambao wameziba masikio yao na kufunga macho yao wasione maovu, wasisikie maovu na wasiseme maovu. Hawakwambii ukweli kuhusu hali ya nchi.

Mshauri anayekufaa ni yule anayekwambia hali halisi ilivyo bila kusita. Huyu ndiye anayekusaidia kutafuta suluhu kwa matatizo ya wananchi.

Ni busara kwa Rais Kenyatta kupuuza shinikizo za wanaomtaka abaki madarakani 2022 kwani hii ni hatari kwake na taifa.