Habari Mseto

NGCDF: Wabunge wakataa chaguo la waziri Yatani

March 18th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne walitupilia mbali uteuzi wa Mohammed Abdille kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NGCDF).

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu NGCDF walichukua hatua hiyo baada ya kubainika kuwa Profesa Abdille, ambaye aliteuliwa kwa wadhifa huo na Waziri wa Fedha Ukur Yatani, alichukuliwa hatua za kinidhamu na Chuo Kikuu cha Maasai Mara.

Wanachama wa Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Igembe Kaskazini Maore Maoka, waligundua kuwa mteule huyo alikuwa amesimamishwa kazi Novemba 2019 katika chuo hicho ambako alihudumu kama msaidizi wa Naibu Chansela (DVC).

“Kamati hii imebaini kuwa Profesa Abdille alisimamishwa kazi kama Msaidizi wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara mnamo Novemba 15, 2019, kwa tuhuma kadhaa ikiwemo kutwaa mali ya chuo kinyume cha sheria. Kwa hivyo, huyu ni mtu ambaye maadili yake ni ya kutiliwa shaka,” Bw Maore akasema bungeni Jumanne alasiri.

Bw Yatani alikuwa amemteua Profesa Abdille kuchukua pahala pa Yusuf Mbuno ambaye amehudumu kama kaimu Afisa Mkuu Mtendaji kwa kipindi cha miaka minane.

Katika barua ambayo iliwasilishwa kwa Kamati hiyo ya Bunge, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Maasai Mara anamtaja Prof Abdille kama mtu mwenye maadili ya kutiliwa shaka.

Kwa mujibu wa Bw Ochola, Profesa Abdille alisimamishwa kazi kutokana na mienendo mibaya, kuchochea wanafunzi na wafanyakazi, matumizi mabaya ya mamlaka ya ofisi yake, kuajiri wafanyakazi kinyume cha sheria na kutomheshimu Naibu Chansela Kitche Magak.

Chuo hicho pia kinamtuhumu Profesa Abdille kwa kutwaa, bila idhini, sehemu ya zulia ambayo ilikuwa ikitumiwa kukarabati ukumbi wa mkutano katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara.

Ikiwa kikao cha bunge lote kitaidhinisha hatua ya kamati hii inayoongozwa na Bw Maore, Waziri Yatani atalazimika kupendekeza jina jingine miongoni mwa yale ambayo yaliwasilishwa kwake na Bodi ya NGCDF.