Michezo

Ngecha FC yaona vimulimuli dhidi ya Kabati Youth

February 25th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KABATI Youth FC iliipepeta Ngecha FC kwa mabo 2-0 katika mechi safi ya Aberdare Regional League, iliyoandaliwa Uwanja wa Mukerenju, Kaunti ya Murangá.

Chipukizi wa Kabati Youth chini ya kocha wake Stephen Odhiambo, walijitupa dimbani kwa kishindo kikubwa huku wakijipenyeza kwenye ngome ya wapinzani bila huruma.

Vijana wa Ngecha kutoka Limuru, watajilaumu wenyewe kwa kupoteza wakati wao mwingi kwa chenga nyingi zisizo na maana.

Iwapo wangetuliza boli chini wangefanikiwa kukabiliana vyema na wapinzani wao.

Tayari katika dakika ya 28 mvamizi matata wa Kabati Youth, Amos Mbogo alichomoka na boli kwa ustadi mkubwa aliwaweka kando madifenda wawili huku akituliza kimiani bao la kwanza.

Huku wakichezea Uwanja wao wa nyumbani vijana a Kabati Youth walipata msisismko kutokana na mashabiki wao waliowashangilia vilivyo.

Kipindi cha lala salama vijana wa Kabati Youth walirejea dimbani kwa kishindo huku lengo lao kuu likiwa ni kuwatafuna wenzao mzimamzima kabla ya kuzoa alama zote tatu.

Straika matata Samuel Aneze alichomoka na boli katikati mwa uwanja na kuonyesha umahiri wake wa soka na bila kupoteza muda aliachilia dhoruba tosha kimiani na kuihakikishia timu yake ushindi wa alama tatu.

“Vijana wangu walifanya kweli kuikomoa Ngecha ambayo imekuwa ikidai kuwa itatunyorosha. Hata hivyo upepo ulibadilika na kwa kweli ushindi ukawa wetu,”alisema kocha Odhiambo.

Alisema timu yake inaaongoza jadwali la Ligi hiyo kwenye kikundi A na alama 7 .Timu ya Muchatha FC ni ya pili na alama 6. Vijana wa Ngecha wanajivunia kuwa na  pointi 5. Halafu Jungle Nuts na Thika Cloth Mills FC zinashikilia alama sawa ya alama 4.

Kocha Odhiambo alisema hata ingawa wanakamata nafasi ya kwanza hawatalegeza kamba hata mara moja lakini watajaribu wawezavyo kutulia hapo kileleni.

Alisema licha ya kuwa na upinzani mkali katika Ligi hiyo bado wanalenga kuibuka na ushindi ifikapo mwishoni mwa Ligi hiyo.