Makala

NGILA: Afrika imethibitisha inaweza kujitegemea yenyewe

August 15th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita, Umoja wa Afrika (AU) ulizindua teknolojia ya kisasaa kuhakikisha hakuna mlipuko wa maambukizi zaidi ya Covid-19 wakati ambapo mataifa mengi barani yanarejelea safari za ndege.

Ili kuwapa imani abiria wa ndege kuhusu usalama wa kiafya wanapozuru mataifa ya kigeni, shirika hilo limeshirikiana na sekta ya kibinafsi kuunda jukwaa la kidijitali la kufuatilia watu waliotangamana na wagonjwa wa virusi vya corona.

Mradi huo kwa jina PanaBIOS, ambao tayari unatumika nchini Ghana kuzuia kukusanyika kwa watu huku pia ukiwezesha safari za mipakani ambapo unawapa wasafiri vyeti vya kuthitbitisha hawana virusi hivyo, umeleta bara hili imani kuwa si lazima litegemee mabara mengine kutatua changamoto.

Kwa kutumia teknolojia hiyo ya kuchanganua data, mataifa mengi yataweza kufanya uamuzi wa busara kuhusu kufungua uchumi.

Teknolojia hiyo ina uwezo wa kufuatilia watu katika mikusanyiko, waliosafiri katika mataifa mengine na hivyo kutoa ramani kuhusu jinsi virusi hivyo vinasambaa.

Inatarajiwa kuwa kila taifa hapa barani litapendezwa na teknolojia hiyo kwa kuwa hakuna anayetaka kulipuka kwa virusi hivyo tena. Visa vyote hapa Afrika vilitoka mabara mengine, na iwapo hatutachukua hatua, kufunguliwa kwa uchumi huenda kukaongezea kusambaa kwa Covid-19 hapa barani kutoka mabara hayo tena.

Lakini la muhimu ni kuwa kuvumbuliwa kwa mradi huo kumethibitisha kuwa bara hili ambalo kwa miongo mingi limekuwa likitegemea misaada ya kiteknolojia kutoka mataifa ya kigeni, sasa lina uwezo wa kuunda suluhu zake na kuzisambaza bila malipo.

Ingawa Afrika bado ina vizuizi vya ukuaji wa teknolojia kama vile bei ghali ya intaneti na uhaba wa simu za kisasa, imejitengenezea suluhu ambayo haihitaji muunganisho wa intaneti kufuatilia waliotangamana na wagonjwa wa Covid-19.

Hii ni ishara tosha kuwa wavumbuzi wa Afrika wamekomaa na kujiamini kutumia teknolojia za data kiasi cha ya kufuatilia watu moja kwa moja kwa simu zao.

Mataifa ya kigeni ambayo yametumia mfumo sawa kubashiri kiwango cha kusambaa kwa virusi ni Uingereza, Israeli na Ujerumani.

Mfumo huo huwaarifu watu ambao wamekuwa kwa hatari ya kuambukizwa virusi hivyo na kuwashauri wapimwe. Watumizi wanaweza kuona matokeo yao na kupewa vyeti vya kuwaruhusu kupita mipakani.

Cha msingi ni kuwa kufuatiliwa kwa wanaotangama na wagonjwa wa corona kutasaidia serikali kubadilisha mwenendo wa Wakenya ambao bado wanakusanyika na kupuuza kanuni.

Kuwatumia arafa ya simu kwamba wametangama na mtu anayeugua corona kutabadilisha tabia yao na hivyo kuwashawishi kusalia nyumbani na kufuata maagizo ya serikali.