Makala

NGILA: Afrika ipakie taarifa zake mitandaoni kukabili ukoloni wa kiakili

October 9th, 2018 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

MSOMI wa masuala ya mawasiliano Nancy Fraser katika nadharia yake kuhusu uundaji wa dhana za fikra alikusudia kuelezea kuhusu ukosefu wa usawa katika kushirikishwa kwa watu wote kuunda mitazamo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mataifa mengi hapa barani Afrika yanaongoza katika tofauti za kiuchumi kwa kuwa yanashuhudia pengo pana baina ya walalahoi na mabwanyenye.

Ingawa suala hili linaathiri pakubwa maendeleo ya kiuchumi Afrika, Kenya ikiwemo, serikali nyingi hulipuuza zinapounda sera na ajenda zake za kitaifa.

Sote twajua kuwa ukosefu huu wa usawa wa kiuchumi hujitokeza wazi katika jamii, lakini pia unaonekana mitandaoni ambapo wale wanaodhibiti taarifa na data za intaneti wanatawala na kueneza fikra na mienendo ya kijamii na kiuchumi.

Matukio ya mitandaoni kupitia posti za Facebook, Twitter, Instagram na tovuti kadha huunda dhana na fikra ambazo huzua midahalo inayoleta mitazamo na mienendo inayokubalika katika maisha nje ya mitandao.

Mambo mengi yanayokubalika katika Dunia ya sasa huanzishwa, huchongwa, kuundiwa mbinu za ushawishi na kupigiwa debe mitandaoni.?Kinaya ni kuwa Afrika, licha ya kuwa na watumizi wengi wa taarifa za mitandaoni, huchangia chini ya asilimia moja ya taarifa zinazosomwa katika intaneti.

Hii ina maana kuwa Afrika bado iko chini ya wakoloni kwa kuzembea kushiriki katika uundaji wa fikra za kilimwengu katika enzi hizi za dijitali. Waafrika husoma taarifa za Wazungu wanazoamini kuwa kweli.

Hivyo, utaiona Afrika ikipinga mambo ya ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja lakini haifanyi chochote kubadilisha zile fikra za mataifa ya mabara mengine ambayo yanaamini kuwa ushoga ni haki ya kibinadamu!

Mitazamo

Licha ya kuwa na wapenzi wengi zaidi wa mitandao barani Afrika, Kenya iko nyuma sana katika shughuli nzima ya kubadilisha mitazamo kuhusu tamaduni za kisasa ambazo Wakenya huziona kuwa zisizofaa.

Wako wapi Wakenya wanaomiliki blogu za kubalisha fikra za walimwengu kuhusu ushoga? Ziko wapi taarifa za kina kwenye tovuti, makala mapana ya video, grafiki na picha za kuelezea hatari za kukubali utamaduni wa Kiafrika kumezwa na wakoloni wa mitandaoni?

Mitazamo yetu ni duni. Kila Mkenya ukimuuliza kuhusu suala hili atajitetea kuwa hilo ni jukumu la wanahabari. Mabara ya Amerika, Ulaya na Asia hayategemei wanahabari kamwe yanapounda taswira za kilimwengu.

Wakenya wanafaa kutumia uwepo wao kwa wingi mitandaoni kulinda tamaduni za Kiafrika na wala si kupayuka kwa hamaki tu wanapoona filamu kama vile ya Rafiki ikiteuliwa kwa Tuzo za Oscar.

Iwapo bara hili linathamini utamaduni wake, wakati wa kuanza kupakia mitandaoni habari za kulinda mitazamo yake ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ni sasa.