Makala

NGILA: Ithibati tele uhaba wa chakula utasuluhishwa na teknolojia

August 7th, 2018 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

HATUA ya hivi majuzi ya kampuni ya Safaricom kusajili wakulima 150,000 wa Kaunti ya Makueni katika programu ya simu ya DigiFarm ni ithibati tosha kwamba tatizo la uhaba wa chakula nchini linaweza kukabiliwa kikamilifu kupitia teknolojia za kisasa.

Programu hiyo itawawezesha wakulima kupata mbegu, fatalaiza, vifaa vya shambani na dawa za kuzuia magonjwa ya mimea popote walipo, kwa bei nafuu katika mabohari matatu katika kaunti hiyo.

Safaricom ilianza kuwaelimisha wakulima hapo Juni kuhusu jinsi ya kutumia programu hiyo, mpango uliofanikishwa na jitihada za kaunti hiyo za kuhakikishia wakulima maisha bora.

Kando na kuweka miundombinu ya kuzalisha mazao bora, wakulima pia wataunganishwa na masoko na wanunuzi moja kwa moja, hali itakayofungia nje mawakala na mabroka wenye mazoea ya kuongeza bei za mazao.

Ingawa mradi huo umejaribiwa katika maeneo mengine nchini ambako DigiFarm ina mabohari 18, wakati umefika kwa Wizara ya Kilimo kuomba ushirikiano na Safaricom kueneza teknolojia hiii katika maeneo yote humu nchini.

Manufaa ya teknolojia hii yatatambulika na wananchi iwapo itawasaidia moja kwa moja kuboresha mbinu zao za uzalishaji pamoja na kuwainua kiuchumi.

Kufikia sasa, mradi huu umesajili wakulima 700,000 lakini nchi yetu ina wakulima zaidi ya milioni tano.

Uenezaji wa teknolojia huchukua muda, lakini serikali za kaunti zote zinafaa kuanza kuweka mazingira bora ya ukuaji wa teknolojia hii maanake kila mwekezaji hupenda mazingira yatakayositiri biashara yake, na Safaricom haitapenda pahali ambapo fedha za umma zinafujwa.

Si wazo zuri kwa wakulima maeneo ya Pwani au magharibi kusikia kuna teknolojia inayoweza kuwasaidia kukabiliana na mabroka walaghai wenye uroho wa kuvuna zaidi kuliko wakulima, lakini teknolojia hiyo iwe haipatikani.

Mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za serikali ni kuhakikishia Kenya chakula cha kutosha kinachozalishwa humu nchini, na chakula hicho kipatikane kwa bei nafuu.

Hivyo, DigiFarm ni programu itakayopiga jeki ajenda hiyo, lakini haiwezekani iwapo Wizara ya Kilimo itazidi kuzembea kuhusishwa katika uvumbuzi huu.

Kila mkulima hupenda kutumia mtaji wa chini na kuvuna pesa za maana, na hii ndiyo teknolojia itakayoinusuru nchi hii, si kutokana na baa la njaa pekee, bali pia kutokana na viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa ajira.

Iwapo mradi huu utatekelezwa katika kila kaunti nchini, matatizo mengi ya kiuchumi kama mfumuko wa bei, bei ghali ya mazao, fatalaiza, mbegu na vifaa, mavuno duni na ukosefu wa soko yatayeyuka. Wakulima wa matabaka yote lazima wafundishwe jinsi ya kutumia programu hii.

[email protected]