Makala

NGILA: Jubilee ikabiliane na visiki hivi ili kutimiza Ajenda Nne Kuu

February 14th, 2018 2 min read

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wahutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi. Picha/ Maktaba

Na FAUSTINE NGILA

Kwa Muhtasari:

  • Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo 
  • Mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote
  • Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake
  • Wakenya wanakumbana na gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa na utovu wa usalama

SERIKALI ya Jubilee imekariri kuwa itaunda zaidi ya nafasi 1.29 milioni za ajira kutokana na viwanda kufikia mwaka 2022.

Hii ina maana kuwa kwa wastani, serikali itaunda nafasi 706 kila siku ili kutimiza ahadi hiyo. Katika mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, serikali inalenga kuimarisha sekta za viwanda, afya, ujenzi na kilimo (chakula).

Kufikia mwishoni mwa 2018, utawala wa Jubilee unalenga kuongeza idadi ya wananchi wenye bima ya afya kutoka milioni 16.53 hadi milioni 25.74.

Serikali pia inapanga kujenga nyumba 500,000 itakazokodisha kwa bei nafuu katika miji mikuu kufiki 2022, mpango ambao inasema utaunda nafasi 350,000 za kazi.

Katika sekta ya ngozi, Rais Uhuru Kenyatta anadhamiria kufanikisha utengenezaji wa viatu milioni 20 nchini kufikia 2022, na kuongeza mapato kutokana na mauzo ya kigeni hadi Sh50 bilioni.

 

Mwelekeo wa hasara

Lakini tukirejelea matukio ya kisiasa humu nchini – kuanzia hatua ya kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga kulishwa kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’, hadi mbinu za utawala wa Jubilee za kuzima wazo la marais wawili, Mkenya ataelewa kuwa mwelekeo ambao taifa hili linafuata ni wa hasara kwa wananchi wote.

Katika hali ya sasa ya kisiasa, huenda tukawa na chaguzi mbili sambamba iwapo matatizo yaliyopo hayatasuluhishwa kufikia mwaka 2020.

Hii ndiyo taswira ambayo haifurahishi wengi, lakini ni ithibati kuwa tulicho nacho kwa sasa hapa Kenya, ni changamoto kuu za uongozi katika pande zote za kisiasa, ambazo ni mwiba katika ndoto ya Ajenda Nne Kuu.

Changamoto hizi zinaonekana wazi katika upande wa Rais Uhuru Kenyatta – ikilinganishwa na Bw Raila Odinga – kwa kuwa Rais ndiye nahodha halisi wa chombo hiki kuhusu usimamizi wa ujenzi wa taifa.

Lakini lazima kama Wakenya tutoe maoni yetu kuhusu suluhu ambazo zitaturejesha katika njia bora ya ukuaji wa demokrasia na uchumi.
Mwanzo, sote twafaa kukubali kuwa tuko chini ya katiba, na wala si juu yake.

Tukirejelea kipengee cha 10 cha katiba na mambo yanayoshikilia taifa letu la kidemokrasia, tutapa kuwa tunafaa kuwa na uzalendo, umoja, ugatuzi wa mamlaka, sheria, demokrasia na kuwashirikisha wananchi.

 

Ubinadamu wa taifa

Kuna yale mambo ambayo yanashikilia ubinadamu wa taifa kama heshima, usawa, haki za kijamii, ushirikishi, haki za kibinadamu, kutotenga wengine na kulinda matabaka ya chini.

Mengine kama maadili, uwazi na uwajibikaji yanaashiria utawala bora.

Utawala wa serikali unafaa kutambua kuwa amani hutokana na haki na si kinyume chake, na kwamba haki inahitaji usalama kwa mkono mmoja na haki zetu kwa mkono wa pili.

Pili, ni kuhusu kuimarisha uchumi wa nchi. Fikiria kuhusu utawala ambao unaangazia kupanua uchumi, maliasili, maarifa na utangamano baina ya jamii mbalimbali.

Kwa sasa, tunashuhudia watu wengi wenye ujuzi na maarifa lakini wamegawanyika katika misingi ya kisiasa. Hii haiwezi kusaidia katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu.

 

Ukosefu wa usawa

Tatu, kuna ukosefu wa usawa – matajiri dhidi ya walalahoi – ambao hutokana na kukiukwa kwa mambo manne – usawa wa jinsia, usawa wa maeneo, umri na kushirikishwa kwa jamii zote.

Fikiria kuhusu matatizo ya kila siku yanayowakumba Wakenya – gharama ya juu ya maisha, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa, utovu wa usalama.

Hizi ndizo changamoto ambazo Ajenda Nne Kuu za utawala wa Jubilee unafaa kuangazia kwa kina na kuleta sera mwafaka na mipango tekelezi kuzipunguza.

Kenya ikifuata haya hadi 2022, kwa yakini, haitapoteza dira na itapiga hatua kadha katika kuunda nafasi za ajira zipatao milioni 1.29.