Makala

NGILA: Kampuni ziheshimu taarifa za siri za Wakenya

August 21st, 2018 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WAKENYA wamechoshwa na mtindo wa baadhi ya kampuni za humu nchini na kimataifa kuhifadhi taarifa zao za siri na kuzitumia kwa njia isiyofaa kujinufaisha.

Lakini sasa sheria imependekezwa kulinda taarifa za Wakenya dhidi ya kampuni za kibinafsi na mashirika ya kiserikali yenye mazoea ya kutumia taarifa hizo kujiimarisha kiuchumi.

Ni hali sawa iliyochangia Muungano wa Ulaya (EU) kuweka sheria kali za kulinda usiri wa data za raia wa mataifa 28 wanachama hapo Mei 25 mwaka huu. Na sasa wananchi wa bara hiyo huhisi salama wanapovinjari intaneti.

Hapa nchini, kampuni nyingi hukusanya data kuhusu wateja wake ili kuelewa zaidi mahitaji yao ya huduma au bidhaa wanazouza.

Si kosa kukusanya taarifa hizi, lakini kumekuwa na visa vya matumizi ovyo ya taarifa hizo katika miezi ya hivi karibuni, jambo ambalo linahitaji udhibiti wa dharura.

Mashirika mengi kote duniani yamejipata lawamani kwa kuuza taarifa za siri za wafanyakazi, wateja na wauzaji kwa kampuni zingine bila idhini ya watu wenyewe.

Huu ni ukiukaji wa hali ya juu wa haki ya usiri iliyoko katika Katiba yetu. Kisiki kimekuwa ukosefu wa sheria dhabiti ya kuwezesha kampuni husika kushtakiwa.

Lakini sasa ni afueni baada ya mswada kuwasilishwa bungeni kulinda wananchi dhidi ya matumizi ya kiholela ya taarifa zao kama jina, nambari ya kitambulisho, nambari ya simu, kaunti, shule, dini, uso, makazi, na sehemu simu imewekwa wakati unatumia huduma za intaneti. Kila kampuni inafaa kuelezea sababu zake za kukusanya data na iwapo data hizo zitatumika kuunda tawasifu ya vitendo na mienendo ya Wakenya.

Wananchi wanafaa kuruhusiwa kuona data kuwahusu zilizohifadhiwa na kampuni hizi, na kurekebisha taarifa ambazo zina makosa pamoja na kuzuia utayarishaji wa maamuzi kutokana na programu za kompyuta.

Kulingana na mswada huo, ni afueni kuona pendekezo wafanyakazi wa kampuni na mashirika watakaovunja sheria hii wapigwe faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitano.

Mtindo wa kampuni nyingi kutumia data kuhusu Wakenya kana kwamba ni mali yao binafsi lazima ukome. Data kuhusu Mkenya inamilikiwa na Mkenya huyo na ni aibu kwa kampuni kutumia data hiyo kujinufaisha kifedha.

Kila kampuni inafaa kulinda taarifa kuhusu wafanyakazi wake, na iwapo itashindwa kufanya hivyo, itafaa kutozwa fidia ambayo italipwa walalamishi.

Iwapo kampuni inanuia kutumia data hizo kufanya utafiti ikishirikiana na nyingine, wafanyakazi wanafaa kuombwa idhini.

Sheria hii pia inafaa kupendekeza kiwango cha fedha ambacho wafanyakazi wanafaa kulipwa, hasa ikiwa kampuni hiyo inalenga kupata faida kutokana na data yao.