Makala

NGILA: Kenya ifuate mfano wa Israeli kuleta maendeleo

February 4th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

KWA muda mrefu sasa, Kenya imejivunia jina ‘Silicon Savannah’ ya Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa katika ubunifu wa kiteknolojia.

Hata hivyo, taifa hili limeshuhudia vikwazo vingi ambavyo vimezuia kufikia viwango vya kimataifa kama Silicon Valley ya Amerika au Shenzhen ya Uchina.

Lakini ziara yangu nchini Israeli, mojawapo ya mataifa yaliyopiga hatua kubwa kiteknolojia, ilinipa imani kuwa Kenya, licha ya changamoto nyingi, bado inaweza kujinyanyua na kufikia viwango hitajika.

Israeli, kwa mfano, ni ya pili duniani katika mataifa yanayotengea utafiti fedha nyingi kwa kuwekeza asilimia nne ya bajeti ya taifa kwa utafiti wa kisayansi.

Kwa sasa imejizolea jina ‘Silicon Wadi’ kutokana na uvumbuzi wa kipekee katika kilimo, uchukuzi, afya, mawasiliano, fedha, elimu, usalama mitandaoni na hata michezo.

Tofauti na Kenya, nchi hiyo ina asasi husika katika masuala yote ya ubunifu wa kiteknolojia, ambayo hufadhili na kuafuatilia miradi yote ibuka.

Hii inaondoa kizingiti kikuu katika uzinduzi wa miradi au biashara za kiteknolojia, kama inavyofanyika hapa Kenya.

Huku Kenya ikipania kuwatoza ushuru wajasiriamali wa mitandaoni wa zaidi ya asilimia 30, serikali ya Israeli imepunguza kiwango hicho hadi aslimia 5 pekee. Hii imechochea kuimarika kwa uchumi, huku takwimu zikionyesha angalau kampuni 80 huanzishwa kila mwaka.

Kila mtu nchini Israeli ana jukumu la kukuza uchumi katika enzi hizi za dijitali, huku miradi ya wakazi wa matabaka ya chini kama Waislamu, wanawake na wakimbizi wakipewa ufadhili sawa na Wayahudi, wanaume na raia wazaliwa wa Israeli.

Elimu ya chuo kikuu katika miji ya Tel Aviv, Jerusalem na Beer Sheva imevutia wanafunzi kutoka kila pembe ya dunia kwani vyuo hufundisha masuala ya kisasa. Watoto wa kuanzia miaka 10 hufundishwa jinsi ya kuunda program za kompyuta, na wanapokua wananolewa kuhusu mbinu za kisasa za kuzima wadukuzi mitandaoni.

Katika mfumo wao wa vituo 380 vya utafiti, mafanikio yamekuwa mengi maanake asilimia 46 ya mauzo ya kigeni hutokana na teknolojia.

Usisahau kuwa Israeli ni taifa lililo jangwani. Lakini walianza vipi? Kwa kujikubali kama taifa kame, Waisraeli walivumbua mfumo wa kitaifa wa unyunyiziaji maji, uliochochea ubunifu katika sekta zingine.

Mwanzoni, Israeli ilikumbwa na changamoto nyingi kuliko Kenya lakini sasa inatambuliwa duniani kwa bidii yake katika uchumi wa kidijitali.

Hapa Kenya, ni wakati wa kujifunza kutokana na taifa hilo. Asasi husika katika ufadhili wa uvumbuzi zimeonekana kukwama na kufumbia macho uwezo mkubwa tulio nao katika sekta ya dijitali.

Tusipichokua hatua, ukosefu wa mtaji, elimu dhaifu kuhusu mustakabali wa viwanda, sharia hasi, ufisadi, na fedha kidogo zimezotengewa utafiti ni visiki ambavyo vitazidi kuilemaza Kenya kiteknolojia.

Migawanyiko ya kisiasa, kikabila, kiumri, kifedha na kijinsia ni majabali ambayo kila Mkenya anafaa kujitolea kuondoa katika barabara ya ustawi wa uchumi wa kidijitali.

Wanasiasa wetu wanafaa kujikomboa kutokana na shetani wa ubinafsi ambaye amewafanya kujifikiria tu kuhusu maslahi yao ya kibinafsi badala ya jinsi wanavyoweza kusaidia taifa hili kusonga mbele katika kila sehemu ya maisha.

Wakati wa kufuata mfano wa Israeli ni sasa!

Mwandishi ni mhariri mkuu wa tovuti ya Taifa Leo 

[email protected]