Makala

NGILA: Matumizi ya data bila kibali yapasa kuzimwa

January 28th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita tuliwaona wanasiasa wakitumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kujivumisha kisiasa.

Naibu Rais William Ruto, kwa mfano, alitumia runinga ya NTV kufafanua maswali mengi ambayo Wakenya na jamii ya kimataifa inajiuliza kumhusu, huku siasa za Uchaguzi Mkuu wa 2022 zikipamba moto.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga pia naye alitumia jukwaa lilo hilo Jumapili kuelezea masuala kadha kuhusu siasa nchini.

Wakati huo huo, wakili Miguna Miguna alikuwa akielezea masaibu yake katika runinga ya K24, ambapo alisisitiza kuwa mageuzi ndiyo suluhu kwa changamoto za taifa hili.

Lakini wanasiasa hawa wanatambua fika kuwa ingawa Wakenya wengi hawana hela za kununua runinga, watapata habari hizo kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter.

Kivipi? NTV, kwa mfano, ina wafuasi milioni 2.2 kwenye Twitter na milioni 3 katika Facebook.

Kwa ufupi, ujumbe wa wanasiasa hawa huwafikia Wakenya wengi maanake Kenya inaongoza katika umiliki wa simu barani Afrika.

Wasichojua Wakenya ni kuwa kuna makundi ya kisiri ya wachanganuzi wa data ya kisiasa ambayo yanatumia muda wao mwingi kujaribu kuelewa ni maeneo gani yanafuatilia jumbe za wanasiasa hawa, na wanachosema kuwahusu.

Hii hutumika kuwashauri wanasiasa hawa kuhusu mienendo ya wafuasi wao mitandaoni, na kuwasaidia kubashiri jinsi watapiga kura hapo 2022.

Mbinu hii imetumika awali katika uchaguzi mkuu wa Amerika na kura ya maamuzi ya Uingereza maarufu kama Brexit. Matokeo yake yalikuwa sahihi, lakini baadaye wapigakura walilalamika walikuwa wakifuatiliwa mitandaoni.

Hivyo, wachanganuzi wa humu nchini wanapotumia data za watu na mienendo yao mitandaoni ili kuvuna mamilioni ya hela, wanafaa kukumbuka kuwa Kenya sasa ina Sheria ya Data ambayo inalinda siri za wananchi.

Kampuni yoyote inyojaribu kujitajirisha kutokana na data ya kisiasa inafaa kuelewa kuwa wakurugenzi wake wanaweza kutupwa ndani na kulipa faini ya mamilioni.

Katika utumizi wa data yoyote, unapaswa kuomba ruhusa ya kuitumia kwani ni utovu wa maadili, ukora na ujambazi wa kipekee kutumia jumbe za kisiri za watu kubashiri nani atakuwa Rais hapo 2022.

Kwa kuwa Serikali ina vifaa vya kidijitali vinavyohitajika kuzima mbinu hizi, haifai kuzembea kukabili wahusika. Hii ndiyo njia ya pekee ya kulinda demokrasia wakati enzi hizi za mageuzi ya kiteknolojia.