Makala

NGILA: Mazuri ya teknolojia kwa ajira yanazidi mabaya yake

June 18th, 2019 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

JE, umewahi kufikiria kuhusu mustakabali wa ajira katika enzi hizi ambapo teknolojia inakua kwa kasi?

Naam, watu wengi wameelezea jinsi teknolojia itachochea wanadamu kupoteza ajira zao ila bila kuzingatia idadi ya kazi ambazo zitabuniwa na teknolojia hiyo hiyo.

Ni kweli kwamba huenda ajira milioni 75 zikamezwa na teknolojia za kiroboti na kiotomatiki kufikia mwaka wa 2022, kulingana na ripoti ya Jukwaa la Kiuchumi Duniani (WEF).

Takwimu hizi zinawatia hofu wafanyakazi wengi lakini ripoti hiyo pia inabashiri kuwa nafasi milioni 133 za ajira zitabuniwa katika kipindi hicho.

Hizi ni habari njema, lakini kutakuwa na changamoto katika kipindi hicho cha mpito kwa waajiri na wafanyakazi.

Waajiri watahitajika kuwekeza katika teknolojia zifaazo huku nao wafanyakazi wakijitolea kupata ujuzi unaohitajika.

Kufikia 2022, kila mtu atahitaji takriban siku 101 zaidi za kuongeza maarifa ya kiteknolojia, kulingana na ripoti hiyo.

Mambo manne yatawezesha mchakato mzima wa kuongeza idadi ya ajira – intaneti ya kasi ya juu, teknolojia ya kiotomatiki, uchanganuzi wa data kubwa na uhifadhi wa faili kwenye intaneti.

Hata hivyo, mataifa yanayoendelea kama Kenya yanahitajika kufanya nini?

Mwanzo, elimu kuhusu siku za usoni za kila aina ya ajira yafaa kuandaliwa. Miundomsingi ya kuwezesha mpito huu inafaa kuwekwa. Kwa mfano, tunahitaji intaneti ya kasi ya juu katika kila pembe ya nchi, umeme hadi vijijini na barabara kupenyeza katika maeneo mengi ya mashinani.

Ikumbukwe kwamba, teknolojia nyingi kama intaneti hutegemea umeme, ambao usambazaji wake nao hutegemea uwepo wa barabara.

Sayansi ya data inafaa kuwekwa kwenye mtaala wa taasisi na vyuo vikuu, maanake kwa sasa ni nguzo muhimu kwa serikali na kampuni nyingi zinazotaka kuchanganua data nyingi kwa usahihi na bila kupoteza wakati.

Asilimia 54 ya wafanyakazi watahitajika kuelimishwa zaidi ili kupata ujuzi mpya. Kati ya watu hawa, asilimia 35 watahitaji miezi sita zaidi ya mafunzo huku asilimia 9 wakitakiwa kufundishwa kwa hadi mwaka mzima.

Hivyo, ili kuepuka hali hii, Wizara ya Elimu inafaa kuanza kubuni kozi za Sayansi ya Data mapema ili kujiandaa kwa vurugu inayokuja kuhusu ajira.

Serikali Kuu ikishirikiana na kampuni za mawasiliano za Safaricom, Airtel na Telkom zafaa kujizatiti zaidi kueneza mawimbi ya intaneti yenye kasi katika meneo ya mashinani na kwa gharama nafuu kwa watumizi.

Matokeo ya ripoti ya WEF yanafaa kutufungua macho na kuanza kuweka mikakati ya kukabili changamoto za teknolojia kupiga watu kalamu.

Tukumbuke kuwa Kenya ndiyo kiingilio cha teknolojia mpya barani Afrika na hatuna budi kujiweka tayari kuchangia mwamko huu mpya kwa bara zima la Afrika.