NGILA: Serikali isianzishe mradi mpya, ikamilishe Konza

NGILA: Serikali isianzishe mradi mpya, ikamilishe Konza

Na FAUSTINE NGILA

HIVI, una habari kuwa serikali ina mpango wa kujenga jiji lingine la kiteknolojia katika eneo la Athi River licha ya kukwama kwa mradi wa jiji la kisasa la Konza?

Badala ya kujifunza kutokana na mapungufu ambayo serikali imejionea katika mradi wa Konza, sasa, kupitia gazeti rasmi la serikali lililochapishwa Agosti 9, serikali imeahidi Wakenya kuwa itakuwa imejenga nyumba 500,000 kufikia mwishoni mwa 2022.

Mzaha gani huu tena? Tayari, Konza ambayo ilianza kujengwa mwaka wa 2013 haina chochote kuonyesha kuwa mji huo unaleta maendeleo.

Ziko wapi nafasi 20,000 za ajira ambazo waliopendekeza kujengwa kwa mji huo waliahidi Wakenya?

Inamaanisha kuwa serikali ya Kenya kamwe haiwezi kuweka ahadi ya maana.

Kilichopo sasa ni uchapishaji wa jinsi miradi itakavyoendeshwa kwa kipindi fulani, huku maafisa walafi wakisubiria hela za bajeti zitolewe watafune.

Ni nini kilifanyikia mradi maarufu sana wa Galana Kulalu uliosemekana utaondolea Kenya tishio la baa la njaa?

Uroho wa kumumunya mabilioni ya mlipa ushuru bila huruma na kuwaacha mamilioni ya Wakenya kwenye hatari ya kufa njaa ndio uliozima ndoto hiyo.

Kwanini miradi hii isiendeshwe kwa kasi tunayoshuhudia katika baadhi ya miradi kama ule wa SGR ama barabara kuu ya kutoka Westlands hadi uwanja wa ndege wa JKIA?

Rais aangazie masuala hayo na si kushughulikia miradi fulani kwa lengo la kuonyesha wananchi kuwa wakati wa enzi yake, alifanya kazi.

Hivyo, ni hadaa tupu kuwa kufikia mwishoni mwa 2022, kutakuwa na mji wa kisasa unaotegemea teknolojia kujiendesha katika wadi ya Mavoko, Kaunti ya Machakos.

Nimejionea jinsi ambavyo serikali imefumbia macho mradi uliotarajiwa kufungua uchumi wa mashinani kule Konza, jinsi wizara ya Teknohama imegomea kupiga jeki mradi huo, na kung’amua kuwa mradi wowote wa ujenzi wa miji lazima utakwama tu, licha ya kutengewa fedha.

Mbona tusimalize Konza kwanza kabla ya kuanza mji mwingine wa kiteknolojia?

Iwapo Kenya inataka kuvutia wawekezaji pale Athi, basi inafaa kuonyesha kazi safi ya kutamaniwa iliyofanyika Konza.

Tusiwe waongo wa kila msimu wa uchaguzi kuwaambia wananchi mambo yasiyowezekana. Kama ni mji wa kiteknolojia, lazima kampuni na washikadau husika, walio na weledi wa kujenga miji ya kisasa wahusishwe.

Lazima pia majirani wa mradi huo wahusishwe. Kwa kawaida kujengwa kwa mji wa kisasa kunafaa kupandisha bei ya ardhi eneo hilo lakini kama ujenzi huo utasalia ahadi kwa miaka minane kama ilivyo Konza, walionunua basi watakosa wateja.

Kila mradi wa mabilioni unaojengwa unafaa kuinua uchumi wa eneo hilo lakini kama utasalia ndoto, uchumi wa eneo hilo utasalia kuwa chini na wawekezaji watakosa imani na hata kuondoka.

Ni wakati wa serikali kukoma kuchezea akili wananchi. Tayari Wakenya wanajua kutofautisha kati ya maendeleo na mzaha. Mradi wa Konza na Athi ni mzaha tu.

You can share this post!

USWAHILINI: Huu hapa mseto wa milo inayopendwa mno katika...

Bournemouth wamtwaa mshambuliaji Morgan Rogers kutoka...