Makala

NGILA: Tahadhari kuna utapeli wa corona mitandaoni

April 5th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

Tangu virusi vya corona vianze kusambaa kote duniani, usalama mitandaoni umedorora mno.

Wadukuzi wanatumia ujanja wao kunasa nywila (neno-siri) za walio na hamu ya kuelewa virusi hivi kwa kuwawekea mitego ya kubonyeza linki hatari.

Kumeibuka linki zilizobeba mitaliga (virusi vya mtandaoni), zinazotumwa kwenye baruapepe huku zikiwa na ujumbe kama ‘bonyeza hapa upate tiba’, ‘toa msaada wako hapa kusaidia kumaliza corona’, ‘hivi ndivyo unavyoweza kurudishiwa ushuru’, ‘fuata hapa kupata mikakati ya kujikinga’ na ‘virusi hivi sasa vyaweza kuenezwa kwa hewa’.

Kwa kuwa huwezi kutambua kuwa ni mtego, watu wengi duniani wameishia kupoteza akaunti zao baada ya neno-siri zao wanazotumia kufungua akaunti za kifedha kunakiliwa, na kupelekea hela zao kuibwa.

Na si watu binafsi tu, wadukuzi wanatumia linki feki kuhusu corona kupata data za siri kuhusu mashirika ya afya, uchukuzi, mawasiliano, viwanda na bima.

Lugha zinazotumika katika ujambazi huu ni Kiingereza, Kiitaliano, Kifaransa, Kituruki na Kijapani. Hii inamaanisha ni makundi ya wadukuzi na yanalenga mataifa mengi duniani kupata pesa.

Baada ya kutambua kuwa watu wengi duniani wanasaka ramani za moja kwa moja (mbashara) kuhusu vifo na maambukizi mapya mitandaoni, wadukuzi wengine nao wameunda ramani feki ambazo zinamwelekeza mtumizi kupakua mitaliga kwa kompyuta na simu.

Usijaribu kufuata ramani ambazo zinakuomba kufuata linki fulani, fungua ramani katika tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) au mashirika ya afya yanayoaminika, la sivyo utajuta kunyang’anywa usukani wa akaunti zako za mitandaoni na benki.

Nao wakali wa sarafu za dijitali wamebuni sarafu kwa jina ‘Corona’ kwa mfumo unaowapa watumizi fursa ya kubashiri iwapo wale walioambukizwa virusi hivyo watakufa!

Huku wakiahidi kutoa asilimia 20 ya hela zote zinazokusanywa kwa misaada ya kupunguza maambukizi, kupitia kwa shirika la Msalaba Mwekundu, sarafu hiyo ni mtego tu wa kupoteza hela.

Ninatarajia visa vya wakora wa mitandaoni kutumia virusi vya corona kuhadaa watu viongezeke, kwani wengi wanachochewa na pesa, ambazo sasa wamepata njia rahisi ya kuiba.

Hii ni ithibati kuwa wakati vituo vya utafiti vinaposhughulika laili wa nahari kujaribu kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huu, wengine, kwa uzembe na tamaa yao, sasa wanawapunja wanaosaka habari za kina kuhusu maambukizi.

Hapa Kenya, kutokana na udhaifu wetu katika kukabili wadukuzi, naona watu wengi wakipoteza hela zao katika kipindi hiki, iwapo hawatajielimisha ipasavyo na kukaa chonjo.

Usikubali vishawishi vya mitandaoni vinavyokuhadaa kuwa unaweza kurudishiwa asilimia fulani ya ushuru kwa sababu ya corona.

Tunajua kwamba kwa sasa hakuna tiba ya ugonjwa huu, mbona ufuate linki inayokwambia kuwa tiba mpya imebuniwa?

Mwelimishe mwenzio.