Makala

NGILA: Tahadhari, msimu wa habari feki na kuumbuana ndio huu tena

October 3rd, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

TAYARI wanasiasa wote wanaokamia kuingia Ikulu 2022 wamejitokeza na kuanza kujivumisha kwa wapiga kura.

Vile vile, propaganda za kuchafuliana sifa kwenye mitandao ya kijamii nazo zimeanza, huku pande pinzani zikionekana kujikakamua kutuma jumbe nyingi iwezekanavyo kupigia debe mwaniaji wao.

Kile kinachokera ni ongezeko la habari feki zinazoundwa kwa ustadi wa juu mno na kutumwa kwenye vikundi vya kijamii mitandaoni kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter na YouTube.

Tofauti na chaguzi za awali, mtindo wa kuanza kupapurana mitandaoni umeanza mapema mno, kwani bado kuna miaka miwili hadi uchaguzi wa Agosti 2022.

Kwa kawaida, wanasiasa hawa hulipa magenge mitandaoni kuandaa jumbe hizo za kupotosha ili kujinasia wapigakura wengi zaidi, kama njia moja ya kujitangaza kwa umma na kudunisha wapinzani wao. Kwa kweli hii ni mbinu chafu inayonuia kuwakanganya wananchi.

Kwa mfano, video moja ambayo nilitizama imehaririwa ikawa makala ya kuonya wapigakura dhidi ya kumchagua mwanasiasa mmoja kuwa Rais, huku ikiwataka wakumbuke machafuko ya mwaka 2007-8 yaliyowaacha zaidi ya Wakenya 1,300 wamefariki na maelfu kupoteza makao.

Ni video ambayo inalenga kuwaamulia Wakenya mgombea urais anayefaa, kwa kumchafulia sifa mmoja wa wawanaji katika kile tutakiita ‘ukoloni wa kiteknolojia’ ambapo kundi la kisiasa linatumia weledi wa uhariri kujaribu kubadilisha dhana na fikra za wananchi.

Katika picha nyingine iliyohaririwa, makahaba wanaonekana wakimsifia Naibu Rais Dkt William Ruto kwa “kupiga jeki kazi yetu ya uhasla”. Picha hiyo ilipigwa mnamo 2017 miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu kulingana na uchunguzi wetu, na ujumbe kwenye bango walilobeba makahaba hao umehaririwa.

Changamoto katika siasa za Kenya ni kuwa, huwezi kubaini ni kundi lipi la kisiasa lilihariri picha hiyo. Huenda ni lile linalompinga Dkt Ruto au lile linalomuunga mkono.

Ni baadhi tu ya mamia ya jumbe katika mfumo wa maandishi, picha au video ambazo kwa sasa zinasambazwa kila mahali kujaribu kuwapotosha Wakenya ili wapoteze imani na kiongozi wanayepanga kumchagua.

Wahusika hawatumii vigezo kama ni nani anaweza kukomboa nchi hii kutoka kwa lindi la umaskini, ukosefu wa ajira na miundomsingi duni.

Unafaa kujihadhari sana na jumbe zote za kisiasa unazopokea kwenye mitandao kuanzia sasa hadi uchaguzi utakapofanyika. Kuna uwezekano mkubwa kwamba, habari unayomtumia mwenzio ni feki.

Utafiti uliofanyika mapema Julai mwaka huu na shirika la SIMElab Africa ulifuchua kuwa, asilimia 86 ya Wakenya mitandaoni wameona na kusambaza habari feki.

Hivyo, chunguzeni vizuri chanzo cha ujumbe wowote wa kisiasa kabla ya kuuamini na kuanza kuwatumia marafiki zako.

Tunaishi katika dunia ya teknolojia, na tusipobadilisha fikra zetu kuhusu jumbe za kisiasa, huenda mitandao ikatumiwa kuamua ni nani atakuwa Rais.

Mwandishi ni mhariri wa habari katika tovuti ya Taifa Leo

[email protected]