NGILA: Toka mjini, uchumi wa kidijitali umefika vijijini

NGILA: Toka mjini, uchumi wa kidijitali umefika vijijini

Na FAUSTINE NGILA

RIPOTI ya hivi majuzi kuhusu matumizi ya intaneti nchini imefichua kuwa wakazi wa Kaunti ya Mombasa ndio wanafurahia kasi ya juu zaidi ya intaneti kote nchini.

Licha ya kupiku Nairobi, bado inashangaza kuwa wakazi wa Pwani bado wanasafiri kuja jijini Nairobi kusaka ajira.

Wamesahau kuwa dunia imebadilika, na injini ya uchumi wa sasa ni intaneti inayoweza kutegemewa, na badala ya kusafiri hadi jiji kuu kutafuta riziki, wanafaa kusalia nyumbani na kutumia intaneti hiyo kuunda nafasi za kazi.

Kimsingi, iwapo chochote unachohitaji Nairobi unaweza kukipata popote pale ulipo, basi haina maana kugharimika kuenda Nairobi kukitafuta.

Ninapoandika makala haya, niko kwangu nyumbani mashinani ambapo ninatumia mawimbi ya 4G ya intaneti.

Umefika wakati ambapo mtindo wa zamani ambapo ungeambiwa ukimaliza elimu ya chuo kikuu unafaa kuenda Nairobi kusaka ajira umepitwa na wakati.

Ajira nyingi zimegeuzwa na mabadiliko ya kiteknolojia huku nao ugonjwa wa Covid-19 ukichochea hata zaidi matumizi ya intaneti wakati serikali iliagiza kampuni ziruhusu wafanyakazi wafanyie kazi nyumbani.

Ajira katika sekta zote sasa zimetafutiwa suluhisho la kudumu kuwezesha wafanyakazi kuendeleza huduma wakiwa popote duniani, kupitia kwa intaneti.

Mikutano

Mikutano yote ya ofisini sasa hufanywa kupitia programu kama Zoom, Duo, Microsoft Teams au Blue Jeans.

Hivyo basi, huna budi kuhudhuria.Wakazi wa Mombasa wanafaa kukumbuka kuwa wanapoenda Nairobi, wameacha muundomsingi wa maana sana nyumbani.

Kasi ya juu ya intaneti inaamisha kuwa mawasiliano ya video ni imara zaidi, kufuatilia kazi ofisini ni rahisi zaidi, kuagiza bidhaa mitandaoni ni nywee, kupakua video na faili nzito mitandaoni ni haraka, kusaka ajira za mitandaoni ni mteremko, kutibu wagonjwa vijijini kumewezeshwa na kuendeleza elimu ya juu ni rahisi ikilinganishwa na kaunti nyingine ambazo bado hazijaonja kasi hii.

Suala hili haliwahusu wakazi wa Pwani pekee bali Wakenya wote walio na simu za kisasa na wanaoishi katika kaunti zenye intaneti ya 4G. Huku bei ya intaneti Kenya ikiendelea kushuka, sasa unafaa kujua jinsi ya kuunda mkwanja mitandaoni.

Kwa kuwa maeneo mengi mashinani hayajafikiwa na umeme, unafaa kuanza kuwekeza katika vifaa na teknolojia ya umeme kutokana na miale ya jua ambao unaweza kuutegemea wakati wote ikilinganishwa na umeme wa mijini ambao hupotea unapohitajika mno.

Unapofanyia kazi mashinani, kuna gharama nyingi unazoziepuka ambazo ungelipia hela nyingi mjini kama vile kodi ya nyumba, nauli, maji na umeme.

Hii inamaanisha kuwa ukitumia tarakilishi yako mashinani, unaweza kuokoa hela nyingi zaidi ikilinganishwa na mjini, na hivyo kuweza kujiinua kiuchumi upesi.

Kuna tu Wakenya wengi waliokwama mjini eti kwa sababu wanataka kuishi maisha ya hadhi, lakini mifuko yao ni tupu, wanaomba mikopo kila mahali kulipa kodi ya nyumba na kugharimia maisha ya jiji.

Jambo lingine kuhusu maisha ya mashinani ni kuwa utapumua hewa safi isiyochafuliwa na mafuta ya magari na viwanda, utakula chakula bora kisicho na kemikali za majitaka kwani utakuwa umekikuza wewe mwenyewe shambani.

Mageuzi ya Nne ya Viwanda kwa sasa yashaanza kuingia vijijini, usiendelee kulaza damu mjini, utajiri umejaa mashinani. Jiunge na uchumi wa sasa wa vijijini.

You can share this post!

Serikali yataka walimu warudishe ‘karo’ haramu

TAHARIRI: Ibainishwe mbona chanjo inakataliwa