Habari MsetoKimataifaMakala

NGILA: Tusipochunga, taka za kielektroniki zitatuumiza

October 22nd, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita, nilitembelea kituo kinachokusanya taka za kielektroniki nchini Kenya kilichoko eneo la Utawala, Nairobi, kwa jina WEEE.

Taka hizi ni kompyuta, simu, vipakatalishi, runinga, friji, vipiga chapa, chaja, betri, paneli za sola, ambazo zote hazitumiki tena baada ya kuzeeka na kuharibika.

Vyumba mbalimbali vimetengwa kutupa taka mbalimbali za kielektroniki zikiwemo zilizoundwa kwa chuma, kioo, plastiki na nyaya. Licha ya kituo hiki kukusanya taka kwa wingi kutoka kwa kampuni mbalimbali, mashirika ya serikali na wauzaji wa bidhaa zilizotumika, niligundua kuwa hakiwezi kukidhi hitaji kuu la kuhifadhi taka ya aina hii.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira, Kenya hutupa tani 44,000 za taka za kielektroniki kila mwaka, lakini tangu mwaka wa 2012 kituo cha WEEE kimeokota tani 10,000 pekee za taka.

Hii inamaanisha kunaponyesha, taka hizi zilizotupwa ovyo katika maeneo mbalimbali ya mijini huoshwa na maji ya mvua, na kemikali hatari kusafirishwa mitoni ambapo Wakenya hutumia maji hayo kwa kilimo.

Kinachoshangaza ni kuwa Wakenya wengi na hata serikali hawaelewi hatari ya kutupa taka hii kwa njia holela bila mwongozo ufaao. Kuna haja ya dharura kuhamasisha wananchi kuhusu madhara ya mtindo huu.

Vyuma hatari vinapoingia mitoni, hupenyeza kwenye mchanga na maji, na kuzua madhara ya kiafya kama uharibifu wa ubongo, saratani na uharibifu wa njia za uzazi.

Ni asilimia moja pekee ya taka hizi ambayo hutengenezwa upya kwa matumizi nchini Kenya kwa sababu serikali imefumbia macho sekta hiyo kwa kuachia kazi hiyo kituo kimoja.

Ingawa baadhi ya kampuni za kibinafsi kama Safaricom zimekuwa zikikusanya na kuhifadhi uchafu wake, kiwango cha taka za kielektroniki kinazidi kupanuka duniani, huku tani milioni 53.6 zikirekodiwa mwaka uliopita. Kufikia mwaka 2030, huenda kukawa na tani milioni 74 kutokana na hali kwamba vifaa vingi vya kielektroniki vitazidi kutumika.

Ili kusaidia kuoka hali hii, Kenya inahitaji sheria kuhusu taka za kielektroniki, kwani watu wengi hutupa taka ovyo kutokana na kutojua.

Ingawa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imeweka mwongozo wa kutupa taka hii, sheria kuhusu usimamizi wake inahitajika kusaidia kueneza uelewa miongoni mwa wananchi kuhusu changamoto hii.

Wanaotupa taka ovyo wanafaa kupigwa faini, lakini kwa kushirikiana na sekta ya kibinafsi, NEMA inaweza kupigia debe mbinu kadhaa za kuhifadhi taka za kilektroniki huku pia ikufungua nafasi za ajira kwa mamilioni ya Wakenya wasio na riziki.

Pia, ni njia murua ya kuzichochea kampuni za kibinafsi kuwekeza katika biashara ya vituo vya kuokota taka hii, mpango utakaosaidia kupunguza uchafu huu katika mazingira yetu.

Kila Mkenya anafaa kuelewa jinsi ya kutupa taka ipasavyo ikiwa vifaa hivyo vimefikia kilele cha matumizi. Ikiwa unaweza kutumia tena vifaa hivyo kuunda vingine vipya, basi fanya hivyo.

Kenya ni nchi ambayo inaongoza Afrika kwa idadi ya vifaa vya kielektroniki, na iwapo hatutachukua hatua za mapema kupunguza taka kutokana na vifaa hivi, basi tutahatarisha maisha yetu wenyewe.