Makala

NGILA: Tuwape watoto fikra za kutatua changamoto maishani

September 1st, 2019 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari wenye umri wa kati ya miaka minane na 17 katika Kaunti ya Meru walikongamana kupokea mafunzo ya kufikiria kidijitali kutoka kwa waasisi wa mradi wa Code Mashinani.

Wengi walisema wanapendezwa na jinsi teknolojia imeboresha maisha huku wakionekana kuchangamkia masuala ya teknolojia.

Walitaja uanasheria, uanahabari, udaktari, uhandisi na uigizaji kama baadhi ya taaluma ambazo zinawapendeza, huku wakikiri teknolojia itatumika kuboresha kila sekta.

Hata hivyo, afisa mkuu mtendaji wa mradi huo, Jesse Muchai aliwafafanulia kuwa kabla ya kung’amua jinsi ya kuunda programu za simu na kompyuta, wanafaa kuelewa fikra zote zinazochochea kuundwa kwake.

Huu ndio msingi kwani kampuni zote kubwa za teknolojia duniani kama Amazon, Facebook, Google, Twitter au Tesla zilianzishwa baada ya waasisi wake kujiuliza maswali mengi kuhusu dunia ya mbeleni.

Uwezo wa kutambua changamoto kisha kuitafutia suluhu ni nguzo kuu katika maendeleo ya kila taifa duniani. Na ukimfundisha mtoto kufikiria jinsi ya kutatua matatizo, atakuwa mwananchi wa kutegemewa katika uchumi wa nchi.

Na si hilo tu, wanafunzi wanapozoea kukabiliana na visiki, wao huwa wakomavu wa akili na mwenendo wanapohitimu masomo yao. Tatizo tulilo nalo hapa Kenya ni kuwa watoto wanalelewa kwa kubembelezwa, wasijue tabu wala vizingiti maishani. Utawaona wakiitisha wazazi wao vitu kwa lazima na wasiponunuliwa wanatisha kujinyonga!

Tukiendelea kulea watoto wetu hivi watakuwa tu vifyefye maishani, hawatajisaidia kwa lolote wala kujikwamua kwa tatizo lolote. Na kizazi kizima cha usoni hakitaweza kukabiliana na mawimbi ya teknolojia kama 5G, Blockchain na Sayansi ya Data ambazo zitafuta nafasi za ajira zilizopo huku zikiunda zingine mpya.

Wazazi wanafaa kutambua kuwa unapomzoesha mtoto maisha ya kupewa kila kitu bila kung’ang’ana, kumtatulia changamoto zake, yeye huishia kukosa ubunifu ambao unahitajika katika dunia ya sasa iliyojaa ushindani.

Mustakabali wa uchumi wetu kwa sasa umo mikononi mwa ubunifu katika teknolojia. Kwa hivyo, iwapo mwanafunzi wa chuo kikuu atahitimu kwa shahada ya uanasheria na hajui jinsi ya kutumia teknolojia kuwasilisha ushahidi kortini kwa niaba ya mteja wake, atapoteza ajira.

Kuanzia umri mdogo, kama miaka mitano hivi, tunafaa kuwafundisha watoto baadhi ya teknolojia zinazotumika kwa sasa.

Hata unapomnunulia vifaa vya kuchezea, hakikisha vinaimarisha akili yake, mpe changamoto azoee angali mchanga. Akikomaa atakuwa mbunifu kiasi cha kuunda programu za kipekee.

Hivyo, ukomavu wa mtoto unadhibitiwa na wazazi wake. Tusipowafunza jinsi ya kufikiria suluhu za changamoto, basi kizazi kijacho kitakuwa cha watu wazembe wanaotegemea usaidizi wa wazazi, wasioweza kubuni mifumo ya maana inayotoa nafasi za ajira.