Makala

NGILA: Ujio wa Amazon utaboresha uwekezaji mitandaoni

November 11th, 2019 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

TANGAZO la kampuni ya Amerika inayotoa huduma za intaneti na tovuti duniani, Amazon Web Services kuwa itatumia Nairobi kama makao yake ya kusambaza huduma hizo Afrika Mashariki litawafaa wawekezaji wa mitandaoni.

Hatua ya Amazon ni thibitisho kuwa Kenya imo miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa utoaji wa huduma za teknolojia hapa barani, licha ya gharama ya data kuwa juu kuliko viwango vya kimataifa.

Kwa miaka mingi, kampuni za huduma za data hapa Kenya zimekosolewa kwa bei ghali ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya vituo vya teknolojia nchini.

Bei ya seva za tovuti na hifadhi ya data imekuwa ghali mno nchini. Kwa mfano, kampuni moja ya humu nchini ya mawasiliano hulipisha Sh1,100 kwa kila 100GB za kuhifadhi data kwa intaneti.

Ingawa Amazon haijatoa viwango vyake vya malipo ya uhifadhi wa data, kuja kwake kutaleta ushindani mkali ambao utachangia kupungua kwa bei za juu za huduma hizo.

Duniani kote, kampuni hii inaongoza kwa udhibiti wa soko la huduma za mitandaoni, na hivyo kampuni zinazowapunja Wakenya zitakoma kufanya hivyo, kwani inatazamiwa kutikisa soko la humu nchini kwa manufaa ya watumizi wa intaneti.

Wakenya wamechoshwa na kunyanyaswa na kampuni za mawasiliano ambazo huwachezea shere wanaonunua data ya hela kidogo kama Sh20,, kwa sababu data hii huisha katika kipindi cha muda mfupi mno.

Uchunguzi umebaini kuwa kampuni hizi huwapa huduma bora watumizi wanaonunua data ya kuanzia Sh1,000 kwenda juu na kutoa huduma duni kwa wale wasioweza kufikia bei hiyo.

Serikali imekuwa ikiunga mkono udhibiti wa kibinfasi wa bei hii ambao umechochea mtindo huu, lakini sasa kuna matumaini baada ya Amazon kuingia kwenye ushindani, wawekezaji wa huduma za mitandaoni watafaidi pakubwa kutokana na bei nafuu.

Hili likifanyika, miradi mingi ya uwekezaji wa dijitali itafufuka, kwani imebanwa na huduma za bei ghali. Hivyo, inatarajiwa kuwa idadi ya ajira katika sekta ya dijitali ikiongezeka, na mapato yakienda juu zaidi.

Mazingira ya dijitali nchini yatabadilika, na hili litawavutia wawekezaji wa kimataifa kufungua ofisi zao humu nchini. Tayari Nairobi ni kivutio kikuu cha uwekezaji, lakini licha ya kasi ya juu ya intaneti, gharama ya seva za tovuti imekuwa juu.

Kenya imepoteza mabilioni ya fedha kutokana na udukuzi wa mitandaoni, uhuni ambao Amazon, inayomilikiwa na mtu tajiri zaidi duniani, Jeff Bezos, itasaidia kuzima kutokana na tajriba yake ya miaka 13 katika usalama wa mitandaoni.