Makala

NGILA: Ukoloni wa data waja Afrika tusipochukua hatua

August 6th, 2019 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA Biblia Takatifu, (Mathayo 2:1-12) , Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za Mfalme Herode, tunasimuliwa jinsi mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi?”

Katika muktadha huo, jamii nyingi za Afrika zama za kale zilikuwa zikiomba zikitazama mashariki. Ni dhana gani hasa kuhusu hii mashariki?

Kwa sasa tunaishi katika nyakati za teknolojia, ambapo tumeshuhudia ubunifu wa kidijitali ukimiminika hapa barani Afrika kutoka mashariki ya dunia, yaani Uchina, Japan na Korea Kusini.

Teknolojia ya Blockchain kwa mfano, iliasisiwa na mtu au kundi la watu kwa jina Satoshi Nakamoto. Simu ya kwanza ya mawimbi ya 5G ilizinduliwa jijini Beijing, Uchina.

Taifa hilo limepigia debe teknolojia hiyo inayopingwa mno na mataifa ya magharibi, hasa Amerika. Pia teknolojia za uchanganuzi wa data, uchapishaji wa 3D na ubunifu wa kiotomatiki zimekita mizizi nchini humo.

Sisemi kuwa wao ndio ‘mamajusi wa kisasa’, lakini hizi ndizo teknolojia ambazo, kwa mtazamo wangu, naamini zimeundwa kulifaa bara la Afrika kwa kuwa mataifa mengi ya ng’ambo yamepiga hatua kubwa za maendelo ya kiuchumi.

Na mataifa hayo sasa yameng’amua kuwa soko la bidhaa zao za kiteknolojia imo Afrika, hivyo yamekuwa yakizileta kwa wingi.

Lakini wanasera wa Afrika wamezembea kuelimisha bara hili kuhusu mazingira safi yasiyo na uchafu kama Uchina na Ujerumani yanavyoweza kuwafaa watu wake.

Jina ‘Afrika’ lafaa kuwa dhana ya kiuchumi, na hivyo mataifa yote yanafaa kuungana kutumia teknolojia zote ibuka kusuluhisha matatizo yake.

Kwa mafano, tuna uwezo wa kutumia teknolojia hizi kuzima ghasia baada ya uchaguzi, kukomesha ufisadi, kuepusha watu na madhara ya bidhaa ghushi huku tukiimarisha sekta zetu za afya, elimu, fedha, ardhi, utalii, uchukuzi, mawasiliano naviwanda.

Kuna mtindo hapa barani Afrika wa wengi wa wataalamu watajika wa teknnolojia kuhamia mataifa yaliyoendelea kama Uchina na Amerika, na kuajiriwa kuunda programu za kusuluhisha matatizo ya Afrika, kisha kuuzwa Afrika.

Uchina na Amerika hazitakwambia miradi ya teknolojia iliyofeli, zitajipiga kifua kuhusu miradi iliyofaulu. Lakini mradi mmoja ukifeli Afrika, watatuanika kama bara lisilojielewa. Hivyo, wanaohamia mataifa hayo ni maadui wa Afrika.

Ni wakati wa mataifa ya Afrika kutumia teknolojia ibuka kujinyanyua kutokana na umaskini, la sivyo, tutashuhudia ukoloni wa pili kutoka kwa mataifa haya kupitia data.

Tunafaa kutumia teknolojia zao kuchanganua data kuhusu Afrika, kisha kutoa suluhu na kuzitekeleza, kabla ya mataifa hayo yenye uwezo mkuu kiteknolojia kutuvamia na kuchukua usukani wa uchumi wetu.