Makala

NGILA: Ushirikiano kiteknolojia utapunguza maambukizi

September 24th, 2020 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA kipindi ambapo maambukizi ya virusi vya corona yanatarajiwa kuongezeka barani Uropa, ripoti moja ilionya kuwa, iwapo chanjo itapatikana, kuna uwezekano mataifa yaliyostawi yatanunua chanjo bilioni mbili na hivyo kuongezea idadi ya watu wanaofariki kutokana na ugonjwa huo.

Dunia imejaa ubinafsi, ambapo waliojaliwa ukwasi wamekuwa na mtindo wa kununua vitu vyote vilivyoko sokoni kuokoa maisha yao wenyewe, na kuwasahau akina kabwela wasiojiweza.

Tumejionea hayo Kenya pia, ambapo wakati wa upungufu wa unga wa mahindi madukani, wenye hela hukimbia kununua kilo nyingi bila kujali watu wa mapato ya chini pia wana haki ya kuishi.

Licha ya ubunifu mwingi kushuhudiwa duniani katika juhudi za kuzima virusi vya corona, tumeshuhudia suluhu hizo zikiwasaidia watu katika mataifa yenye uchumi imara, huku mamilioni ya raia katika mataifa yasiyojiweza wakiumia.

Kwa mfano, bei ya mashine za kupumua, vifaa vya kupima corona na hata mavazi ya kuzuia maambuikizi imewekwa juu kwa mataifa ya Afrika, huku mashirika machache tu ya kimataifa yakitoa msaada.

Kenya imelalamikia bei ghali ya kupima virusi hivyo, ambayo umehujumu jitihada za kupima watu wengi kama mataifa ya Ameria na Ulaya, ili kujua viwango halisi vya maambukizi.

Kwa kupunguza bei au kutoa misaada kwa Afrika na mataifa yanayoendela, mataifa tajiri yataweza kupunguza idadi ya vifo kutokana na corona.

Lakini hilo halijafanyika kwa kuwa mataifa hayo yanaamini kuwa, yanafaa kutoa msaada wakati corona imeisha katika mataifa yao. Yanasahau kuwa hivi ni vita vya dunia nzima, na kukosa kudhibiti maambukizi katika kila taifa ni njia moja ya kuhakikisha virusi hivyo vitaendelea kudidimiza uchumi wa dunia kwa muda mrefu zaidi.

Naupongeza Muungano wa Afrika kwa kubuni jukwaa la pamoja la mataifa yote 55 kununua dawa mitandaoni bila ubaguzi. Pia, shirika hilo limeunda programu za simu za kuzuia maambukizi mipakani na katika viwanja vya ndege, bila malipo kwa kila nchi.

Ushirikiano wa kimataifa unahitajika mno wakati huu ambapo watu wamefutwa kazi, kampuni zikafunga biashara, shule zinaelea kufungwa hali ambayo imeongezea utovu wa usalama mijini na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Dunia inapotafakari kuhusu njia bora zaidi za kukabiliana na majanga, suala la umoja lazima litiliwe mkazo kwani sisi sote tuna haki sawa ya kuishi, na ukarimu ndio mojawapo ya chanjo dhidi ya virusi hivi, na kurejesha uchumi katika hali ya kawaida.

Teknolojia za kutengeneza chanjo hazitadhibiti maambukizi iwapo zitatumika tu katika mataifa machache.

Licha ya Sh1.9 kwadrilioni kutumika kupiga jeki uchumi wa dunia kufikia sasa, tukiendelea kuwa wabinafsi, huenda tukatumia Sh1.3 kwadrilioni zaidi kufikia mwishoni mwa 2021 kwa kisingizio cha kuokoa maisha. Na hiyo itakuwa hasara kubwa zaidi duniani tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Kufikia sasa, virusi hivi vimesimamisha maendeleo ya miaka 20 kulingana na ripoti hiyo. Huu ndio wakati wa kuwajali wenzetu.