Makala

NGILA: Usimkejeli mwenzio anayetumia simu kusoma Biblia kanisani

August 12th, 2019 2 min read

NA FAUSTINE NGILA

KWA muda mrefu sasa, athari za teknolojia kwa dini zimekuwa zikioneknana kuwa mbaya kwa waumini. Lakini imani hii imekosa kutambua umuhimu uliopo kwa kukumbatia teknolojia makanisani.

Kwa mfano, wakati Mjerumani Johannes Guttenberg alichapisha Biblia kwa mara ya kwanza, alibadilisha jinsi viongozi wa kidini walikuwa wakielewa maandiko matakatifu.

Ubunifu wake huo ulichangia pakubwa katika juhudi za kueneza elimu, na kuwapa wanadamu mtazamo wa kibinafsi kwa Biblia.

Teknolojia ya kisasa si tofauti na ile ya Bw Guttenberg kwani inalenga kurahisisha uelewaji wa vifungu vya neno la Mungu kupitia intaneti, simu za kisasa na mawasiliano ya moja kwa moja.

Watu hujipata wakitumia simu zao wakati wa ibada kanisani humu nchini. Utafiti unaonyesha kuwa wanapohojiwa, asilimia 96 husema haifai kamwe kufanya hivyo.

Lakini wao husahau kwamba kuna programu za vifungu na mistari ya vitabu vya Biblia, ambazo ni rahisi kutumia. Pia wanaweza kuweka posti kwenye Facebook au Twitter za vifungu vinavyogusa nafsi yao kwa wengine kusoma.

Usipumbazwe tena, teknolojia sasa imeyasukuma makanisa kuwa na akaunti katika mitandao ya kijamii ili kufikia waumini wengi zaidi. Video za mahubiri na nyimbo mpya za injili zinapeperushwa moja kwa moja kupitia Facebook kila uchao.

Kulingana na takwimu za Google, watu hutafuta ibada za makanisa mara 30,000 kila mwezi. Ili kufikia watu hawa, kanisa linahitaji kuwa mtandaoni. Ni jukwaa ambalo linaweza kutangaza mambo yake, kuhubiri na kutangamana na waumini moja kwa moja. Wakati muumini amepatwa na jambo la kidharura, ni rahisi kujua kupitia kwa mitandao hiii na kumsaidia.

Kwa makanisa yenye tovuti, waumini hutakiwa kutuma risala zao za maombi kwa makasisi kuhusu changamoto za maisha, na kuweza kuzitatua kupia kwa maombi ya pamoja. Mfano ni muungano wa maumini wa Kanisa Katoliki kwa jina Vincentian Ministries mtaani Lavington, Nairobi.

Kwa wenye maombi maalum, kuna programu za kuwasaidia kuomba na kusoma Biblia. Dropbox inasaidia makanisa kutuma na kupokea nakala za kidini kama mipango ya kanisa, mikutano ya mahubiri na video za mahubiri hayo.

Ilivyo kwa sasa, makanisa duniani tayari yameanza kuwarai waumini kutoa sadaka kupitia majukwaa ya kidijitali. Haitachukua muda mrefu kabla ya mtindo huu kufika hapa Kenya.

Mawimbi ya teknolojia ni mazito, ni vigumu kuyasimamisha na mtu anapokwambia unakosa heshima kwa kutumia simu yako kanisani kusoma Biblia, basi mweleze kuwa mustakablai wa injili umo kwenye teknolojia za kisasa. Huwezi kukwepa.