NGILA: Wanawake barani Afrika wachangamkie teknolojia

NGILA: Wanawake barani Afrika wachangamkie teknolojia

Na FAUSTINE NGILA

INAFEDHEHESHA kwamba hutapata mwanamke hata mmoja kutoka Afrika kwenye orodha ya hivi majuzi ya wanawake 35 wanaomenyana na wanaume kufanikisha utekelezaji wa teknolojia za kisasa.

Waliposherehekea Siku ya Wanawake Duniani, ilikuwa wazi kuwa suala nzima la teknolojia liliepukwa; labda kutokana na dhuluma nyingi tunazoona dhidi ya wanawake, lakini teknolojia ndiyo injini ya dunia ya sasa.

“Ni wakati wa kusema ukweli kuhusu sayansi ya maumbile. Uwezo wa mwanamke na mwanamume hutofautiana kwa sababu za kibayolojia, na tofauti hizi zimechangia pakubwa idadi ndogo ya wanawake katika sekta ya teknolojia.”

Usemi huu wa mhandisi wa kampuni ya Google, James Damore, mnamo 2017 ulisababisha kutimuliwa kwake, aliposhikilia kuwa mapenzi ya wanawake kwenye mahusiano na wanaume yanapunguza uwezo wao katika teknolojia.

Hata hivyo, kutimuliwa kwake hakukubadilisha ukweli huu unaodhihirika katika kampuni nyingi za teknolojia nchini na kimataifa; ambapo asilimia ya wafanyakazi wanawake ni chini ya 30.

Na hili linatokana na hali kwamba wakati idara za nguvukazi zinatangaza ajira za nafasi za kiteknolojia, wanaume ndio hujitokeza kwa wingi kuliko wanawake.

Ni bayana kuwa duniani kote, kozi kama Sayansi ya Kompyuta na Teknolojia za Mawasiliano huvutia wanafunzi wengi wa kiume kuliko wa kike.

Hali hii huishia kuwaathiri wasichana na wanawake kwa jumla, kwani wahandisi wanaounda programu za kompyuta huishia kuziwekea sifa za kiume, na kusahau kuwa zitatumiwa na watu wa jinsia zote mbili.

Ingawa wanawake katika mabara ya Amerika, Ulaya na Asia wanaonekana kujitosa katika teknolojia za kisasa, hapa Afrika ni wachache tu wanapata msukumo wa kuunda programu tajika.

Hivyo, ni wakati wa kuwafundisha wasichana wetu wa Kiafrika, kuanzia umri mdogo, umuhimu wa teknolojia; ili waweze kufurahia na kuenzi uwezo wa kompyuta, na hatimaye kupigania nafasi ya wanawake katika teknolojia.

Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanawapiku wanawake kwa asilimia 12 kote ulimwenguni kwa matumizi ya intaneti, ishara kwamba wanawake hawako tayari kukabili wanaume kupunguza pengo hili katika taaluma ya teknolojia.

Kwa mfano, katika uvumbuzi wa programu za maana humu nchini, zaidi ya asilimia 70 zimeundwa na wanaume.

Kwenye vyuo vya teknolojia, wanafunzi wengi ni wavulana. Katika uanahabari, ni waandishi na watangazaji wanaume ambao wameshamiri katika ulingo wa kuripoti habari na makala ya teknolojia.

Huwezi kulaumu serikali pekee kwa hali hii. Wanawake wanafaa kujitolea wenyewe kuvalia njuga teknolojia, hasa uvumbuzi unaosaidia kutatua changamoto mahususi zinazowakumba; kama vile ukeketaji, ndoa za mapema, dhuluma za kimapenzi na muhimu zaidi, usawa wa kijinsia.

Jukumu hili likiachiwa wanaume litagonga mwamba, kwani kwa kawaida ni vigumu wanaume kujiweka kwenye fikra za kike na kuunda programu za kuwakomboa dada zetu.

Hivyo, ili wasiachwe nyuma, wanawake wanafaa kutambua kuwa dunia ya sasa inaendeshwa kwa teknolojia, na wakati wa mchango wao ni sasa.

Usawa huu wa kiteknolojia utasaidia kuleta usawa wa kijamii.

You can share this post!

WASONGA: Serikali itenge fedha kununua dozi zaidi za chanjo...

GWIJI WA WIKI: Beatrice Gatonye