Makala

NGILA: Wito wa elimu ya Blockchain utaifaa nchi

April 30th, 2019 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

JUMA lililopita, nilihudhuria warsha ya teknolojia katika Chuo Kikuu cha Strathmore almaarufu Nairobi Tech Week ambapo masuala mengi ya kiteknolojia yaliangaziwa na wataalamu mbalimbali.

Mojawapo ya masuala muhimu kwa taifa hili yaliyozungumziwa kwa upana ni teknolojia ya Blockchain.

Wataalamu wa teknolojia hiyo walitoa wito kwa serikali kushirikiana na sekta ya kibinafsi kuelimisha wananchi kuhusu Blockchain, katika juhudi zake za kunasa wezi wa fedha serikalini.

Suala la Blockchain lingali geni kwa Wakenya wengi, na wito huo ni muhimu kueleza jamii maana yake na kwa nini ni muhimu kwa taifa hili.

Ingawa serikali inanuia kutumia teknolojia hiyo katika sekta za afya, ardhi, fedha na elimu, mafunzo na warsha za kila mara ndio njia ya kipekee ya kueneza umuhimu wake.

Haina haja kuanza kutekeleza teknolojia ambayo tayari wananchi hawaielewi, maanake mara nyingi wao huhisi kwamba kuna ukora fulani, na ndio maana hawakuhusishwa.

Tayari kuna mashirika yanayoeneza elimu kuhusu teknolojia hii kwa wataalamu kupitia kwa vyuo vikuu, lakini mwananchi wa mashinani pia anafaa kuelezwa maana yake.

Jopokazi la Blockchain na Teknolojia ya Kiotomatiki lafaa kuweka wazi matokeo ya utafiti wake kuhusu teknolojia hii kwa umma, kabla ya kuwasilisha ripoti kwa waziri wa Teknohama. Ni miezi mitano sasa tangu litangaze limekamilisha utafiti.

Hii ni teknolojia muhimu ambayo ina uwezo wa kuzima ghasia za baada ya kila uchaguzi, kwa kuitumia katika mchakato mzima wa kupiga kura, kuzihesabu na kutangaza mshindi.

Ni uvumbuzi wa kisasa ambao unawafungia nje wadukuzi ambao hunuia kuiba pesa au data za siri za watu, kampuni na serikali kwa kuwa unatambua kila mtu anayeingia mle ndani na kumwanika kwa umma papo hapo.

Baada ya watu kufahamishwa kuuhusu, utaweza kutumiwa kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha za serikali hadi kwenye kaunti, hali ambayo itawaogopesha wezi.

Tatizo la wizi wa fedha za kaunti hutokana na hali kwamba hela hizo hutolewa kutoka Hazina Kuu ambapo huibwa kabla ya kufikia serikali za kaunti, lakini kupitia Blockchain, kila kaunti inaweza kugawiwa hela zake na kufuatiliwa kidijitali.

Itakomesha mazoea ya wanasiasa kutumia wahasibu kuiba pesa kisha kufuta rekodi za wizi huo ili kuficha ushahidi.

Pia, mwenendo wa baadhi ya wafanyabiashara na kampuni kukwepa kulipa ushuru utaisha huku rekodi za Blockchain zikitumika kortini kuhukumu mafisadi.