Makala

NGILA: Yashangaza serikali haina nia ya kutumia tekinolojia kumaliza ufisadi

November 9th, 2019 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

MIEZI mitatu tangu jopokazi la Blockchain kuwasilisha ripoti yake kwa serikali, hakuna kilichotekelezwa au kufanyiwa majaribio kutokana na mapendekezo ya ripoti hiyo.

Licha ya sekta ya kibinafsi kuandaaa makongamano mbalimbali kujadili uwezekano wa teknolojia hiyo kutumika kuboresha utendakazi viwandani na sekta ya umma, serikali yenyewe imeonekana kujikokota kutoa mwongozo au kukubali kuitumia.

Wataalamu wa teknolojia hiyo wamekuwa wakiirai serikali kushirikiana na sekta ya kibinafsi kuelimisha wananchi kuhusu teknolojia hii mpya katika juhudi zake za kuzima ufisadi nchini.

Suala la Blockchain lingali geni kwa Wakenya wengi, na kuzembea kwa serikali katika kuwaeleza maana yake kunashangaza.

Serikali haifai kuogopa kutoa elimu kuhusu teknolojia hii kwa kuwa itanasa maelfu ya wafisadi katika sekta za afya, ardhi, fedha na elimu, na hivyo kuokoa mabilioni ya fedha.

Kenya inafaa kufuata mfano wa Rwanda, ambapo serikali inashirikiana na sekta ya kibinafsi katika teknolojia hii kubuni suluhu kwa changamoto zake.

Tayari kuna mashirika yanayoelimisha wananchi kuhusu Blockchain, lakini serikali inafaa kufadhili elimu hii ili ienezwe hadi mashinani.Jopokazi la Blockchain na Teknolojia ya Kiotomatiki limeweka wazi mapendekezo yake likiamini fika kuwa teknolojia hii itaokoa uchumi wa nchi hii ambo umekumbwa na changamoto.

Ikumbukwe kuwa Blockchain ina uwezo wa kuzima ghasia za nyakati za uchaguzi kutokana na wizi wa kura au uteuzi wa wanasiasa ambao hawajahitimu. Unaweza pia kuitumia katika mchakato mzima wa mchujo, kupiga kura, kuzihesabu na kutangaza mshindi.

Huu ni uvumbuzi wa kisasa ambao unawafungia nje wadukuzi ambao hunuia kuiba pesa au data za siri za watu, kampuni na serikali kwa kuwa unatambua kila mtu anayeingia mle ndani na kumwanika kwa umma papo hapo.

Baada ya watu kufahamishwa kuuhusu, utaweza kutumiwa kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha za serikali hadi kwenye kaunti, hali ambayo itawaogopesha wezi.

Tatizo la wizi wa fedha za kaunti hutokana na hali kwamba hela hizo hutolewa kutoka Hazina Kuu ambapo huibwa kabla ya kufikia serikali za kaunti, lakini kupitia Blockchain, kila kaunti inaweza kugawiwa hela zake na kufuatiliwa kidijitali.Pia itakomesha mazoea ya wanasiasa kutumia wahasibu kuiba pesa kisha kufuta rekodi za wizi huo ili kuficha ushahidi.

Hivyo, serikali inafaa kujitokeza wazi kuhusu mpango wake wa kutumia Blockchain. Bila hivyo, itakuwa rahisi kufikiria serikali inagomea ripoti hiyo kwa sababu itazimia maafisa wake mifereji ya pesa za wizi.