Ngilu aagizwa afike kortini kueleza sababu ya kutolipa madaktari 19

Ngilu aagizwa afike kortini kueleza sababu ya kutolipa madaktari 19

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Kitui, Bi Charity Ngilu, Alhamisi aliagizwa afike kortini Oktoba 14 kwa kukaidi agizo la kuwalipa madaktari 19 mishahara ya miezi minne.

Bi Ngilu hakufika kortini jinsi alivyoagizwa kueleza ikiwa amewalipa madaktari hao alivyoamriwa Oktoba 5, 2021.

Bi Ngilu alikuwa ameagizwa na Jaji Monicah Mbaru wa mahakama ya Kesi za Mizozo ya Wafanyakazi (ELRC) kuwalipa madaktari hao.

Kupitia chama cha madaktari nchini (KMPDU), madaktari hao walishtaki Serikali ya Kaunti ya Kitui na Tume ya Huduma ya Umma ya kaunti hiyo.

KMPDU inaomba mahakama kuu ikomeshe hatua ya serikali ya Kaunti ya Kitui ya kuwatimua kazini madaktari hao.

Chama hicho, kupitia kwa wakili Henry Kurauka kilimweleza Jaji Mbaru kuwa walalamishi hawajalipwa kwa miezi minne tangu Julai 1, 2021.

Bw Kurauka alieleza korti kuwa walalamishi hawakuelezwa sababu ya mishahara yao kusimamishwa na serikali ya kaunti hiyo.

Julai 1, 2021 mahakama ilielezwa kuwa madaktari hao waliokuwa wamekubaliwa kusafiri nchi za nje kwa masomo zaidi walitakiwa warudi kazini.

You can share this post!

Wakazi wakeketwa na njaa mifugo ikizidi kuangamia

Olunga butu Harambee Stars ikiona vimulimuli dhidi ya Mali