Ngilu ahimiza Kalonzo amuunge Raila mkono

Ngilu ahimiza Kalonzo amuunge Raila mkono

Na PIUS MAUNDU

GAVANA wa Kitui, Bi Charity Ngilu amemtaka Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka atupilie mbali azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022, na badala yake amuunge mkono kwa mara ya tatu kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bi Ngiliu anamtaka Bw Musyoka awapuuze wandani wake ambao wanamhimiza awe debeni na badala yake awashauri vinara wenzake ndani ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wamuunge mkono waziri huyo mkuu wa zamani.

Viongozi wengine ndani ya OKA ni Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi wa chama cha Kanu.

Aidha, Bi Ngilu alisema Bw Musyoka kwa mara nyingine anafaa akubali kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga ili kuimarisha nafasi yao ya kuingia ikulu huku akieleza matumaini yake kuwa wataungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

“Ndugu zetu Musyoka, Mudavadi, Wetang’ula na Moi wanafaa waje pamoja kisha washauriane na Bw Odinga kuhusu 2022 na wamuunge mkono ili waunde serikali ijayo,” akasema Bi Ngilu.

Alisema mgawanyiko kati ya wanasiasa hawa utampa nafasi nzuri Naibu Rais Dkt William Ruto kuwashinda uchaguzini huku jamii ya Akamba ikiendelea kusalia kwenye baridi kisiasa.

“Japo tunahitaji Bw Musyoka kuwa katika serikali ijayo na kuwa rais, hatuna kura za kutosha za kumwezesha kutimiza azma yake. Tayari mchakato wa kubadili katiba kupitia BBI umeanguka kwa hivyo tunafaa tuwaze upya jinsi tutakavyojipanga kuelekea 2022,” akaongeza.

Gavana huyo alikuwa akizungumza katika kijiji cha Uthiuni, Kaunti ya Makueni wakati wa mazishi ya nduguye Mzee Samuel Mutuku ambapo baadhi ya wanasiasa walitumwa kuwasilisha rambirambi za Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kauli ya Bi Ngilu inajiri wakati ambapo wanasiasa wa Wiper wamemtaka Bw Musyoka kuwania urais kivyake iwapo wanasiasa wenzake ndani ya OKA hawatamkabidhi tiketi ya kuwania kiti cha urais.

Pia wabunge hao wakiongozwa na Rachel Nyamai wa Kitui Kusini kwa tiketi ya Jubilee, walisema Bw Musyoka ndiye kiongozi mwenye maono ambaye anaweza kufikisha nchi hii mbali kimaendeleo.

Bi Nyamai alifichua kuwa alitumwa na Rais Kenyatta kuwaeleza Wakamba kuwa Bw Musyoka ndiye chaguo lake 2022 na wanafaa wahakikishe umoja wa jamii hiyo, makamu huyo wa rais wa zamani anaposaka uungwaji mkono maeneo mengine.

You can share this post!

Kinara wa Arsenal atetea matumizi ya fedha ya kikosi hicho...

Baba ndani kwa madai ya kumchoma mwanawe