Habari MsetoSiasa

Ngilu atia makali madiwani wakipanga kumng'atua uongozini

June 17th, 2020 2 min read

Na BONIFACE MWANIKI

GAVANA wa Kitui, Bi Charity Ngilu amesemekana kuanza juhudi za kuvunja serikali hiyo baada ya habari kumfikia kuwa madiwani wameanza mchakato kutaka kumng’atua mamlakani kwa shutuma za utumizi mbaya wa mamalaka.

Hayo yanajiri wakati ambapo Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru anangoja hatima yake kuhusu hoja ya kung’olewa mamlakani.

Kwa muda mrefu sasa, mtafaruku mkubwa umeshuhudiwa baina ya serikali ya Bi Ngilu na bunge la kaunti hiyo, huku madiwani wakimshtumu gavana kwa kutowajibika na ubadhirifu wa pesa.

Hata hivyo, Bi Ngilu kwa upande wake amekuwa akikishtumu Chama cha Wiper kinachoongozwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, kilicho na madiwani wengi zaidi katika bunge la Kitui.

Gavana huyo hudai kuwa chama hicho kimekuwa kikwazo kikubwa katika juhudi zake za utendakazi.

Imefichuka kwamba, siku chache zilizopita, madiwani wa kaunti hiyo walikusanya sahihi za wawakilishi wadi 35 wakiwa na nia ya kumng’atua Bi Ngilu mamlakani kwa madai ya kutowajibika, na utumizi mbaya wa mamlaka.

Kisheria, sahihi 34 ndizo zinahitajika ili kuruhusu kujadiliwa kwa hoja ya kumng’atua gavana huyo mamlakani.

Bi Ngilu anaonekana kuchukulia kwa uzito suala hilo, na sasa kupitia kwa chama chake cha NARC ameanza mchakato wa kukusanya sahihi kutoka kwa wakazi wa Kitui kwa nia ya kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kubandua kaunti ya Kitui na kuweka uongozi wa kaunti hiyo mikononi mwa serikali kuu.

Mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Kitui, Bw Miltonic Kitute, mnamo Jumatatu alisema kuwa muda umewadia wa Rais Kenyatta kuwaokoa wakazi wa Kitui kutoka kwenye mzozo wa kiuongozi, ambao umewanyima maendeleo kwa muda mrefu sasa.

“Ni wazi kuwa bunge la Kitui liko tayari kuhujumu utendakazi wa Gavana Ngilu, na ni lazima tusitishe juhudi zao zenye nia mbaya kwa wakazi wa kaunti hii,” Bw Kitute aliambia gazeti la Taifa leo.

Alieleza kusikitishwa kwake na jinsi ambavyo madiwani wamekuwa wakihujumu uongozi wa Bi Ngilu tangu alipochaguliwa, akirejelea tukio la hivi majuzi ambapo bunge la kaunti hiyo lilikataa majina ya wanachama wa bodi ya utumishi wa umma katika kaunti.

Hatua ya chama cha NARC, inakuja wiki kadhaa baada ya Bi Ngilu kumsuta kinara Bw Musyoka kwa madai kuwa amekuwa akitumia madiwani kuhujumu utawala wake.

“Madiwani wa Wiper wamekuwa wakitumia wingi wao bungeni kuhujumu utawala wangu kwa kutopitisha miswada yangu ya kimaendeleo. Niko radhi kusema kuwa kinara wa Wiper lazima anahusika, kwani hawakanyi madiwani wake hata baada ya kufanya hivyo,” alieleza Bi Ngilu.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Bi Ngilu alimshinda mgombeaji wa Wiper, Bw Julius Malombe na tangu hapo hakujakuwa na amani kati yake na wafuasi wa Wiper.

Mtafaruku huu sasa umewasha moto wa kisiasa katika kaunti ya Kitui, huku viongozi wa chama cha NARC wakisema kuwa hawatokubali kinara wao ang’atuliwe mamalakani bila kuwaadhibu wahusika wakuu.