Ngoingwa, mtaa unaoimarika kwa kasi Kiambu

Ngoingwa, mtaa unaoimarika kwa kasi Kiambu

NA SAMMY WAWERU

Kiambu ni mojawapo ya kaunti zinazounda eneo la Mlima Kenya na ni tajika katika shughuli za kilimo na ufugaji, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika majumba ya kupangisha.

Kaunti hiyo pia ina viwanda kadha, vya maziwa na uongezaji thamani wa zao hilo vikiongoza.

Mtaa wa Ngoingwa, Thika unapatikana katika kaunti ya Kiambu. Ukizuru eneo hilo utalakiwa na mandhari ya hadhi ya juu kutokana na majumba ya kifahari yaliyojengwa.

Hata ingawa mengi ni ya kibinafsi, kuna kadha ya kupangisha ili kusitiri wenye mapato ya kadri na yale madogo.

Ni katika eneo lilo hilo barabara kuu inayoungisha mji wa Thika na Limuru na Naivasha imepitia.

Zaidi ya miaka kumi iliyopita mengi ya mashamba mtaa huo yalikuwa uga wa kahawa, zao ambalo sasa kwa wakulima wa Mlima Kenya limetelekezwa na serikali.

Chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais (mstaafu) Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kahawa na majanichai yalikuwa yameimarika. Hata hivyo, kufuatia kupuuzwa kwa mazao hayo, soko likitajwa kuwa duni, baadhi ya wakulima wameamua kuchukua hatua nyingine.

Wamiliki wa mashamba Ngoingwa, ni miongoni mwa waliochukua hatua hiyo, wengi wakiingilia uwekezaji wa majumba ya kupangisha. Aidha, yamegawanywa kwa makundi; waliojenga makasri yao, ya kukodi, na ya ghorofa ya kupangisha.

Kulingana na Bw Eric Mutunga, ambaye amewahi kuhudumu kama keateka wa mojawapo ya ploti, wengi waling’oa miti ya kahawa – mikahawa, ili kufanya shughuli za ujenzi. “Bei ya kahawa ilipoanza kuzorota, walianza kung’oa mikahawa ili kuwekeza katika majengo ya kupangisha,” anasema Mutunga.

Kwa mujibu wa shirika la Kenya Nairobi Coffee Exchange (NCE), Kenya huuza zaidi ya asilimia 95 ya kahawa katika mataifa ya kigeni. “Licha ya kahawa kudaiwa kununuliwa vizuri huko nje, wakulima wanaumia na ndio sababu wengi wanang’oa miti yake ili kutafuta njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha,” Bw Mutunga aeleza.

Katika mtaa wa Ngoingwa, kuna esteti za kifahari kama vile Chania, Kisiwa, Bidii, miongoni mwa zingine.

Miundomsingi eneo hilo imeimarishwa, ikiwamo barabara, shule, zahanati, hekalu za kuabudu, na hata kituo cha polisi.

Ni katika mtaa uo huo, barabara inayoelekea Limuru, Naivasha na Nakuru, maarufu kama Ngoingwa – Mang’u Road imepitia. Ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka mjini Thika, serikali kuu inapania kutengeneza barabara ya njia nne (dual carriage) sawa na Thika Super Highway, itakayopitia eneo la Ngoingwa na Mang’u, kutoka Thika hadi Limuru.

Ni kufuatia kuimarika kwa miundomsingi eneo hilo ambapo bei ya mashamba na ploti imekwea mlima. Kipande cha ardhi chenye ukubwa wa thumni ekari (1/8) hakipungui Sh1.2 milioni. “Mwaka 2010 nilitaka kununua ploti yenye kimo cha futi 40 kwa 80, kwa Sh600 sikupata, nililazimika kununua kwingine. Sasa bei ya ploti na mashamba humu Ngoingwa haikamatiki,” Irene Wanjiru, mfanyabiashara akaambia Taifa Leo Digitali.

Isitoshe, eneo hilo lina mikahawa ya kifahari pamoja na maeneo ya burudani kama vile vilabu na mabaa.

Kutoka barabara ya Ngoingwa – Mangu, kuingia maeneo ya ndani, hata ingawa njia hazijawekwa lami, zimeimarishwa na vijigari vidogo aina ya tuktuk vinatumika kufanikisha shughuli za usafiri na uchukuzi.

Katika makasri ya mabwanyenye, kuna wanaofanya ufugaji wa kuku, kilimo cha matunda kama vile ndizi na ukuzaji wa viazi asilia kama mihogo.

Mashamba yaliyo ndani, hususan karibu na chemichemi za maji yanakuzwa mboga, nyanya, vitunguu, pilipili mboga na hata viazi vikuu. Eric Mutunga hukuza mboga za kienyeji kama vile mnavu almaarufu sucha au managu, mchicha (terere) na kunde. Bw Mutunga pia hulima spinachi na sukuma wiki.

“Ngoingwa ni eneo lililojaaliwa, kuanzia uwekezaji wa majengo ya kupangisha, makasri ya kifahari na kilimo. Tunakula chakula cha mazao safi yaliyotoka shambani moja kwa moja,” afafanua mkulima huyo. Anasema wengi wa mabwanyenye eneo hilo huendea mazao shambani. “Oda zao zimeniwezesha kununua pikipiki ili kuwafikishia mazao,” adokeza.

Hata ingawa, ni wachache mno wanaokuza kahawa, huenda shinikizo la mapato bora ya majengo ya kupangisha yakawashawishi kubadili mawazo yao. Sekta ya biashara pia inaonekana kunoga, hasa vipuri vya magari na vifaa vya ujenzi.

Ili kuimarisha uchumi wa eneo hilo, Jeremiah Njuguna mtaalamu wa masuala ya kiuchumi na mhasibu katika benki moja nchini anasema muhimu ni kusawazisha ada ya nyumba za kukodi na kuishi na vilevile za biashara kuwa za bei nafuu. “Wawekezaji huvutiwa na mandhari na mazingira wanayomudu na yaliyo salama kwa biashara zao,” ahimiza Bw Njuguna.

Mtaalamu huyo pia anasisitizia usambazaji wa maji safi na ya kutosha, ambayo eneo la Ngoingwa si balaa kwani yamesheheni.

You can share this post!

MATHEKA: Ofisi ya DPP izingatie utaalamu kukusanya ushahidi

OBARA: Agizo la Rais kuhusu wabunge mawakili lilijaa unafiki

adminleo