Habari Mseto

Ng'ombe 16 waibwa watu wawili wakipigwa risasi Samburu

October 4th, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

Watu wawili walipigwa risasi na kuuawa huku ng’ombe 16 wakiibwa Jumatatu jioni wakati wavamizi walivamia Kijiji cha Natiti, Baragoi Kaunti Ndogo ya Samburu Kaskazini.

Wawili hao walivamiwa na wezi wa mifugo wanaoaminika kuwa majirani wao walipokuwa wakichunga ng’ombe eneo la Natiti.

Kamanda wa polisi wa Samburu Kaskazini Tom Makori aliambia Taifa Leo kwamba wawili hao walifariki papo kwa hapo.

“Washambulizi hao walivamia  wawili hao na kuwapiga risasi baada ya kuiba ng’ombe hao,” alisema Bw Makori.

Alisema kwamba polisi walikuwa wanawatafuta wawili hao na kwamba usalama umeimarishwa eneo hilo.

“Tutahakikisha kwamba usalama umeimarishwa na hatutapumzika mpaka tuhakikishe kwamba wavamizi hao wamekamatwa,” aliongeza.

Mkuu huyo wa polisi aliwwaomba wakazi wawape maafisa wa usalama wafanye uchunguzi na wawakamate wavamizi hao.

Aliwaomba wakazi wakiwa na taarifa zozote kuhusu wavamizi hao wasikose kuwaambia maafisa wa usalama ili wakamatwe.

Bw Makori aliomba jamii tofauti ziiishi na majirani wao kwa amani waepukane na mizozo.