Habari Mseto

Ng’ombe walivyogeuka kuwa kero kwa wafanyabiashara Nairobi

September 12th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

NG’OMBE huthaminiwa kwa ajili ya maziwa na nyama; bidhaa ambazo ni sehemu ya lishe ya kila siku.

Ngozi yake pia inatumika katika uundaji wa bidhaa mbalimbali.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara – hasa wa bidhaa za kula Kaunti ya Nairobi wanaouzia kandokando mwa barabara – wanatoa malalamiko kwamba mifugo hiyo inawahangaisha hasa ng’ombe wanaporuhusiwa kuzurura kiholela.

Wauzaji wa bidhaa kama mboga, matunda na hata viazi wamesema hawakosi kukadiria hasara inayosababishwa na mifugo hao.

“Kuna ng’ombe wanaoachiliwa kujitafutia lishe na wamekuwa kero kwa sie wafanyabiashara tunaouza bidhaa za kula hususan za mbogamboga,” akalalamika mama nmoja anayeuza mboga, matunda na karoti eneo la Roysambu wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Kuna baadhi ya wakazi wanaofuga ng’ombe Nairobi na kwa sababu ya uhaba wa mashamba kukuza nyasi za mifugo, huwafungulia kujitafutia lishe kandokando mwa barabara.

Hata ingawa kuna wanaoandamana na wachungaji, wafanyabiashara tuliozungumza nao walisema hawajali bidhaa za watu.

“Hata wakila hawatufidii hasara tunayokadiria,” akasema muuzaji wa viazi mtaani Zimmerman.

Malalamiko hayo ni sawa na ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa za kula barabarani eneo la Githurai.

Katika barabara za mitaa mbalimbali Nairobi na Kiambu, hutakosa kutazama ng’ombe wakivuka.

Mwaka 2018 mbunge mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Kiambu Gathoni Wa Muchomba alikuwa ameahidi kuwasilisha mswada bungeni kuangazia suala la wakulima Kiambu na Nairobi kuhangaishwa na ng’ombe wanaoachiliwa kujitafutia chakula kiholela.