Habari MsetoSiasa

Ngome ya Ruto yapasuka vipande vitatu

August 9th, 2020 2 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

VUGUVUGU jipya la kisiasa lanukia katika ngome ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto, eneo la Rift Valley.Hii ni kufuatia mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa Kiongozi wa KANU, Bw Gideon Moi kuhusu muungano wake wake na Jubilee.

Wakosoaji wa Dkt Ruto ambao walikuwa wameungana na mwenyekiti wa Kanu sasa wamekerwa na ushirikiano kati ya Seneta huyo na Rais Uhuru Kenyatta na wanapanga kubuni vuguvugu lingine la kisiasa la ‘kutetea masilahi ya jamii’.

Wakiongozwa na Mbunge wa Cherangany Joshua Kuttuy, wanasiasa hao wanamkashifu Gideon kwa kutumia ushirikiano kati ya Jubilee na Kanu kuendeleza masilahi yake ya kibinafsi wala sio ya jamii pana ya Wakalenjin.

Wengine ambao wamemgeuka Seneta huyo wa Baringo ni wabunge; Alfred Keter (Nandi Hills), Silas Tiren (Moiben) na mwenzao wa Emurua Dikkir Johanna Ng’eno.

Hata hivyo, Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos amemtetea Seneta Moi akisema ushirikiano wake na Rais Kenyatta umeleta ‘manufaa’ Rift Valley.Kuttuny na wenzake waamemgeuka mwenyekiti huyo wa Kanu wakati ambapo ameimarisha juhudi za kujinadi kisiasa katika eneo hilo ambako Dkt Ruto ana ushawishi mkubwa.

Mnamo Ijumaa Mbunge huyo wa Cherangany alimshutumu Seneta Moi kwa kuchochea kutemwa kwa maafisa wa serikali kuu kutoka Rift Valley wanaosawiriwa kumuunga mkono Dkt Ruto.

Bw Kuttuny alisema yuko tayari kukatiza uhusiano wake na mwenyekiti huyo wa Kanu kwa kuwaadhibu “watu wetu wasio na hatia” kwa kisingizio cha kumpiga vita Naibu Rais.

Hata hivyo, mbunge huyo alishikilia kuwa ataendelea kuuunga mkono Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.“Gideon amekuwa akiwatisha watu wetu ambao waliteuliwa katika nyadhifa mbalimbali serikalini kutokana na ushawishi wa Naibu Rais Dkt Ruto.

Kwa hivyo, ikiwa itabidi nitalikiane naye, niko tayari kwa sababu hawezi kuendelea kuwaondoa wataalamu wetu kutoka nyadhifa za uwaziri na zile za mashirika ya serikali ili nafasi zao zipewe na marafiki zake,” Bw Kuttuny akafoka.

Akaongeza: “Haja yangu kuu ni kuendeleza masilahi ya watu wetu. Na hii ndio maana nitasalia kuwa mwaminifu kwa Rais na, mwenzake katika handisheki, Bw Odinga na hivyo sijajiunga na kambi ya Naibu Rais.”

Bw Kuttuny vile vile alipasua mbarika kwamba hivi karibu “mrengo wa tatu” utabuniwa katikaka Rift Valley utakaoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Wengine, akaeleza, watakuwa viongozi wenye maono sawa kama vile aliyekuwa mgombeaji wa ugavana Uasin Gishu Zedekiah Bundotich (Buzeki) na wabunge Tiren, Keter.

Ufichuzi kuhusu uwepo wa mgawanyiko ndani ya kambi ya Seneta Moi unaashiria kuwa atakuwa na kibarua kigumu katika jitihada zake za kupigania ubabe wa kisiasa dhidi ya Dkt Ruto katika Rift Valley kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kila mmoja wa viongozi hao kutoka jamii ya Kalenjin atajizatiti kutumia udhaifu wa mwenza akisaka ushawishi miongoni mwa mamilioni ya wapiga kura katika eneo hilo pana.

Kwa muda wa miaka 10 iliyopita Dkt Ruto amekuwa ndiye mwenye usemi kisiasa, akionekana kumlemea Seneta Moi.Lakini mabadiliko yaliyolifanyika katika ulingo wa siasa za kitaifa majuzi na hatua ya Kanu kubuni muungano na Kanu, yamemkweza Seneta Moi na kuimarisha ushawishi wake katika eneo hilo.