HabariSiasa

Ngome ya Ruto yapasuka

May 8th, 2019 2 min read

Na CLIFF KIPSANG na JEREMIAH KIPLANG

?Ngome ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto eneo la Rift Valley imeanza kuyumba huku wanasiasa kadha kutoka sehemu hiyo wakijitenga na vuguvugu la Tangatanga linalompigia dede Dkt Ruto.

Hata hivyo,wandani wa Dkt Ruto jana walijitokeza kuwapuuzilia mbali wanasiasa waliogura kambi yao hivi majuzi wakiwataja kama watu wanaojishughulisha na siasa zisizo na maana.

Walisema madai ya mfanyabiashara Zedekiah Bundotich Kiprop, almaarufu Buzeki na Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos kwamba walihama wiki jana kwa sababu ya kuzuiwa kumfikia Dkt Ruto hayana msingi wowote.

Mbunge wa Soy, Caleb Kositany alisema Naibu Rais anaweza kufikiwa na viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa bila changamoto yoyote.

“Hizi ni siasa za pesa nane. Hakuna mtu ambaye amezuiwa kumwona Naibu Rais. Kwa hakika hatuwezi kusema lolote kuhusu Buzeki kwa sababu hajawahi kuwa pamoja nasi baada ya kuwania ugavana kama mgombeaji huru. Kwa hivyo hajamwacha Naibu Rais,” Bw Kositany akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu.

Akitangaza kujiondoa kutoka kambi ya Dkt Ruto wiki jana Bw Buzeki, ambaye ni mfanyabiashara tajiri katika kaunti ya Uasin Gishu, alisema alichukua hatua hiyo baada ya kuhisi kudunishwa na baadhi ya wandani kigogo huyo.

Alisema ameamua kufuata mkondo wake mwenyewe kisiasa, huku akiajiandaa kuwania ugavana wa Uasin Gishu katika uchaguzi mkuu wa 2022. Bw Buzeki alishindwa kwa kura chache na Gavana Jackson Mandago katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Naye Bw Tolgos ameamua kuungana na kambi ya Seneta wa Baringo Gideon Moi ambaye ni hasidi mkuu wa kisiasa wa Naibu Rais katika eneo la Rift Valley.

Mnamo Jumatano, Bw Tolgos ambaye amekuwa akishiriki vita vya kisiasa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, alisema ameamua kutojiunga na kundi la “Tanga Tanga” akilitaja kama lililosheheni viongozi wenye “matusi na ujeuri.”

Bw Murkomen, ambaye ni kiongozi wa wengi katika seneti, naye alipuuzilia mbali madai ya gavana huyo akiyataja kama ya kupotosha.

“Wajibu wangu mkuu wakati huu ni kuwatumikia watu wa Elgeyo Marakwet kwa kushughulikia kero la utovu wa usalama katika bonde la Kerio. Siwezi kujibizana na viongozi waliopoteza mwelekeo kama Gavana Tolgos,” akasema Bw Murkomen.

Wiki jana, Bw Tolgos aliungana na Seneta Gideon kuwapokea kiongozi wa ODM Raila Odinga na kakake Oburu Oginga walipozuru Kabarak kumpa pole Rais mstaafu Daniel Moi kufuatia kifo cha mwanawe, Jonathan Toroitich.

Hii iliashiria kuwa, gavana huyo anayehudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, amejiunga na Kanu kinachopinga ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu. Mwanasiasa mwingine kutoka Uasin Gishu aliyetangaza kujitenga na kambi ya Dkt Ruto ni Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Bi Glady Shollei.

“Hautaniona katika mikutano ya makundi yaTanga Tanga au Kieleweke. Hii ni kwa sababu nimejitolea kushughulikia ajenda ya maendeleo wala sio siasa. Kwa hivyo sitapoteza muda wangu kuzunguka na makundi haya kila mara,” akasema Bi Shollei, siku chache baada ya Buzeki kujitenga na kambi ya Dkt Ruto.

Na Gavana Mandago pia ameonekana kujitenga na kampeni za kumpigia debe Naibu Rais akionekana kujishughulisha zaidi ya masuala ya kaunti ya Uasin Gishu. Majuzi, aliwaonya wakazi wa kaunti hiyo dhidi ya kujishughulisha na masuala ya siasa “ili msiumie na kuvunjika moyo.”

Wabunge wengine kutoka Rift Valley ambayo wamejiunga na kambi ya wanasiasa wanaopania kuzima ndoto ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta ni; Silas Tiren (Moiben), Alfred Keter (Nandi Hill), William Kamket (Tiaty) na Mbunge wa Baringo ya Kati Joshua Kandie aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC).