Ngozi Okonjo-Iweala: Mwanamke na Mwafrika wa kwanza kuongoza WTO

Ngozi Okonjo-Iweala: Mwanamke na Mwafrika wa kwanza kuongoza WTO

CHARLES WASONGA Na AFP

GENEVA, Uswizi

NI rasmi sasa kwamba Mnigeria Ngozi Okonjo-Iweala ndiye mwanamke na Mwafrika wa kwanza kushikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) baada ya kuteuliwa rasmi Jumatatu.

Okonjo-Iweala aliteuliwa katika mkutano maalum wa baraza kuu la mataifa wanachama wa WTO ulioendeshwa kwa njia ya mtandao wa Zoom. Mkurugenzi mkuu huyo mpya aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha nchini Nigeria na mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB) kanda ya Afrika.

Akiongea punde baada ya kuteuliwa, Bw Okonjo-Iweala, 66, alisema kuwa WTO chini ya uongozi wake itachangia pakubwa katika mpango wa ufufuzi wa chumi za mataifa wanachama kutoka na changamoto zilizosababishwa na janga la corona.

“WTO thabiti na yenye nguvu ni muhimu zaidi ikiwa tutajimboa kutoka kwa athari zilizosababishwa na Covid-19,” afisa huyo ambaye ni mwanauchumi aliseme kwenye taarifa.

“Natarajia kufanya kazi na mataifa wanachama kuandaa na kutekeleza mikakati ya kisera tunayohitaji kurejesha uchumi wa ulimwengu katika mkondo wa maendeleo tena. WTO inakabiliwa na changamoto nyingi lakini tukifanya kazi kwa ushirikiano tunaweza kuifanya kuwa thabiti na yenye nguvu tena na inayoweza kukabiliana na changamoto za kisasa,” akaeleza.

Okonjo-Iweala ataanza rasmi kazi mnamo Machi 1, na muhula wake utaendelea hadi Agosti 2025. Anaweza kupewa nafasi kuhudumu muhula wa pili ikiwa mataifa wanachama wataafikiana kuhusu jambo hilo.

“Hakuteuliwa kwa sababu yeye ni mwanamke au kwa sababu anatoka Afrika, lakini kwa sababu…. Alijitokeza kwa mwaniaji bora kwenye uhitimu, ujuzi na sifa hitaji kwa kazi hii kubwa,” akasema mwanadiplomasia mmoja kutoka mataifa ya Magharibi.

Shirika la WTO lenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswizi, limekuwa bila Mkurugenzi Mkuu baada ya Mbrazil Robeeto Azevedo kujiuzulu mnamo Agosti mwaka jana, mwaka mmoja kabla ya muhula wake kukamilika rasmi

WTO yenye mataifa 164 wanachama huteua viongozi wake kwa njia ya muafaka. Lakini mwaka jana, wagombeaji wanane walioamba kazi hiyo akiwemo Mkenya Balozi Amina Mohammed. Mchujo ulifanywa na wakasalia wawaniaji wawili; Okonjo –Iweala na Yoo Myung-hee ambaye ni raia wa Korea Kusini.

Utawala wa aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump ulimpendelea Myung-hee na kupinga uteuzi wa Okonjo-Iweala.

Lakini mnamo Februari, Myung-jee ambaye ni Waziri wa Biashara Korea Kusini alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho baada ya kubainika kuwa Rais mpya wa Amerika Joe Biden angemuunga mkono Okonjo-Iweala.

“Amerika ina hamu ya kufanya kazi na Dkt Okonjo-Iweala kuhakikisha kuwa WTO inatekeleza wajibu wake kama asasi inayoendeleza ukuaji sawa wa uchumi kupitia biashara,” mwanadiplomasia wa Amerika David Bisbee akaambia mkutano wa baraza kuu la shirika hilo Jumatano.

Okonjo-Iweala ni sasa anakuwa Mkurugenzi Mkuu was aba tangu WTO ilipoasisiwa mnamo 1995.

You can share this post!

BBI: Madiwani wataka kikao na Uhuru, Ruto

IMF kukopesha Kenya Sh262b kufufua uchumi