Makala

NGUGI: Kanisa linachangia matatizo ya kifamilia nchini

February 13th, 2018 2 min read

Biblia Takatifu.Kanisa likikomesha vita na ung’ang’aniaji vyeo makanisani, jamii itapata mahala pema pa kujipatia chakula cha kiroho. Picha/ Maktaba

Na MWITHIGA wa NGUGI

Kwa Muhtasari:

  • Kwa muda sasa tumekuwa tukipata visa mbalimbali vya kinyama kati ya wanandoa
  • Ni aibu sana kuwaona wanadini wakipigana na kushambuliana kanisani kwa maneno
  • Viongozi wetu wanapozivunja sheria za nchi na kukaidi mahakama zetu, huwa tunapanda mbegu za ukaidi
  • Kanisa likikomesha vita na ung’ang’aniaji vyeo makanisani, jamii itapata mahala pema pa kujipatia chakula cha kiroho

Licha ya kuwa na madhehebu mengi yanayohubiri neno la Mungu nchini, inasikitisha kuona uozo ukiendelea kuongezeka kila uchao katika jamii.

Boma nyingi zinazidi kuporomoka kutokana na kutoelewana kwa wanandoa. Kana kwamba mlango wa jehanamu umefunguliwa na kumpa ibilisi nafasi ya kurandaranda atakavyo duniani, kwa muda sasa tunaendelea kupata visa mbalimbali vya kinyama kati ya wanandoa.

Kuna wale wanajitoa uhai eti kwa sababu wapenzi wao wako na ‘mipango ya kando’, huku wengine wakiripotiwa kuangamiza familia yote eti kisa na maana ikiwa ni mizozo ya kimapenzi.

Lakini kabla ya kuisuta jamii na uozo wake, sitosita kukielekeza kidole kingine kwenye baadhi ya makanisa. Vita na malumbano makanisani leo si jambo la ajabu haya yote yakitokea kutokana ung’ang’aniaji wa uongozi.

 

Aibu

Ni aibu sana tunapowaona wanadini wakipigana na kushambuliana kanisani kwa maneno. Tusisahau hawa ndio watu ambao wanafaa kuwa kielelezo chema katika jamii na kwa hivyo wanapoingiza siasa duni za malumbano kanisani kwa hakika huwa wanayadhalilisha madhabahu matakatifu ya Mungu.

Si mara moja Wakenya wamepigwa na butwaa wanaposikia visa vya mapasta kupatikana madanguroni na hata wengine wao wakishtakiwa kwa ubakaji wa watoto wadogo.

Mifano kama hii inapojitokeza kutoka kwa “wachungaji wa kondoo wa Mungu” basi na tutarajie nini kutoka kwa wananchi wa kawaida? Mtoto umleavyo kwa kawaida ndivyo akuavyo, kama jamii tunafaa sote kujilaumu kwa kudorora kwa maadili.

Viongozi wetu nao hawajaachwa nyuma kwa kuchangia ungezeko la ‘mmomonyoko’ wa kimaadili tunaoshuhudia. Si ajabu kamwe kuwaona na kuwasikia viongozi wa kisiasa wakitupiana cheche za matusi kandamnasi ya umma, huku watoto wetu wakipata nafasi ya kujifundisha misamiati mipya na miovu. Isitoshe, siasa za taifa letu nazo zinaendelea kuyazorotesha maadili ya kizazi cha leo.

 

Mbegu za ukaidi

Kwa mfano viongozi wetu wanapozivunja sheria za nchi na kukaidi mahakama zetu, huwa tunapanda mbegu za ukaidi ambazo hatimaye zitazaa matunda ya uharibifu na machafuko.

Jamii yetu haifai kuachiliwa kuzama kwenye bahari kuu ya upotovu bali sote tunafaa kuwa walinzi wa wenzetu. Kila mmoja wetu anafaa kufanya juu chini kuwa mfano bora kwa watoto wetu.

Nalo kanisa lichukue nafasi yake kwa ukamilifu. Naamini vile vile kanisa likikomesha vita na ung’ang’aniaji vyeo makanisani, jamii itapata mahala pema pa kujipatia chakula cha kiroho.

Ninayo ndoto kuwa siku njema kwa jamii yetu yaja, wakati ambapo kila mmoja ataongozwa na maadili mema. Penye nia naamini siku zote pana njia, tusikate tamaa.

[email protected]