Makala

NGUGI: Mabinti wa kisasa wakome kuwananyanyasa waume katika ndoa

September 1st, 2019 2 min read

Na MWITHIGA NGUGI

MKUKI kwa nguruwe siku zote huwa ni mtamu lakini kwa binadamu huwa ni mchungu.

Wakati mtoto wa wa kike anapofanyiwa masihara, ulimwengu mzima huamka na machungu ya kila aina. Lakini mtoto wa kiume anapolawitiwa kelele kwa kweli haziwi nyingi kiasi hicho.

Haya yote yanapofanyika, vita huwa ni dhidi ya dhuluma ya mtoto wa kike.

Kama jamii, kuna mengi tunajaribu kuyakalia kimya, mabwana wanachapwa na wake zao lakini kwa kuogopa aibu, wanaume wanapopelekwa mbele ya machifu na polisi, wao hukubali lawama za kuzua vurugu nyumbani kwao na wengi wao wanaozea jela kama si hospitali ya Mathare.

Wakati umefika wa kuacha upumbavu wa kimawazo sisi kama wazazi, na kujua kwamba watoto wetu wa kiume wanapitia mengi machungu mikononi mwa mabibi zao.

Boma, naamini kwamba huwa hazijengwi na mitutu ya bunduki na pingu za askari, lakini hili limegeuzwa na mabinti wa kisasa kuwatesa waume zao huu wote ukiwa ni utumwa wa ndoa za kisasa.

Badala ya ndoa kuwa furaha kwa wachumba, imekuwa karaha kwa wengi. Mara kwa mara, tunasikia mabwana wengi wakifa katika hali ya kutatanisha na ukiangalia kwa undani, utapata ni kutokana na mali ya familia au mapenzi haramu ya wachumba.

Juzi, tulishuhudia mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu akikatwakatwa na mpenziwe eti kwa sababu ya usuhuba.

Ama kweli kama hizi si dalili za mwisho wa dunia basi hata mimi sijui katu mwisho wa dunia utakuja vipi.

Heshima kati ya wana ndoa imekosa, mabwana wanazomewa kandamnasi ya watu na hata kudhalilishwa mbele ya watoto wao.

Na kutia msumari kwenye kidonda, wake wanatumia polisi kama ngao ya maovu yao kuwakandamiza waume zao bila haya.

Tukitaka kukiponya kidonda cha familia, hususan mauaji yanayotokana kati ya wana ndoa, hebu na kwanza tusuluhishe mizozo ya mara kwa mara kati yao, na pili wazazi wachukue nafasi ya kuwasikiliza watoto wao wa kiume wanapolia ndani ya ndoa.

Korti zetu pia na ziwape nafasi wanaume kusikilizwa ipasavyo kabla ya kufanya maamuzi yake. Hii ni kwa sababu kuna wanaume wengi wanazidi kuozea jela kwa tuhuma tele za wake zao ilhali kama ukweli ungewekwa peupe, wangekuwa watu huru.

Hata hivyo singetaka kuonekana kuwatetea wanaume mwanzo hadi mwisho, lakini usisahau kama walivyosema wahenga, lisemwalo lipo na kama halipo laja, yote tisa, aliyewahi kuumwa na nyoka akiona ung’ongo hushtuka.