Habari Mseto

Ngugi wa Thiong'o ajisajili kwa Huduma Namba Amerika

June 6th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MSOMI Mkenya mtajika Profesa Ngugi wa Thiong’o amejiandikisha kwa mfumo wa Huduma Namba katika ubalozi wa Kenya jijini Los Angeles, Amerika.

Profesa Thiong’o ambaye ni mwandishi maarufu wa vitabu vya Fasihi ya Kiingereza alijindikisha Alhamisi kwa mfumo huo mpya wa usajili wa watu kwa njia ya dijitali (NIIMS) pamoja na mkewe, Njeri wa Ngugi.

Msomi huyu ambaye amefunza katika vyuo vikuu vya New York na Yale miongoni mwa vingine, aliwataa Wakenya wanaoishi ughaibuni kujiandikisha, akisema mfumo huo mpya utaweka msingi ambapo masuala ya maendeleo nchini yatatekelezwa.

Wakenya wanaoishi mataifa ya nchi wamepewa muda wa hadi Juni 20, kujiandikisha katika balozi 54 za Kenya katika mataifa ya nje, kulingana na Wizara ya Mashauri ya kigeni.

Serikali imetuma mitambo 154 ya kieletroniki katika afisi za kibalozi za Kenya ambako usajili huo utaendeshwa.

Humu nchini, shughuli ya usajili ulikamilishwa mnamo Mei 25 mwaka huu ambapo takriban Wakenya 37.7 milioni walisajiliwa.

Mfumo huo wa usajili unanuiwa kuiwezesha serikali kutoa huduma kwa raia kwa njia rahisi.