Makala

NGUGI: Wamchao Mungu wana majukumu zaidi ya kuhubiri

May 30th, 2019 2 min read

Na MWITHIGA WA NGUGI

Kila mja aamkapo na kujiona akiwa mwenye siha, afanyalo kwanza ni kumshukuru Maulana kwa nguvu zake zinazowapa waja wake uhai usiku na mchana.

Na hapa sitosita kuwapa kongole viongozi wote wa dini na madhehebu mbalimbali kote ulimwenguni, kwa jitihada zao za kila wakati za kuwalinda kondoo wote wa Mungu; kwa kuwapa chakula cha kiroho na kuwapa wengi tumaini la maisha na ujio wa pili wa mwana wa adamu.

Makanisani na hata misikitini, mahubiri huwa ni kumtafuta Mungu au Allah kwa minajili ya kutenda haki na kuomba maghufira kila siku.

Hatufai kamwe kusahau viongozi wote wa dini wanafaa kuwa kwenye mstari wa mbele kuzikosoa na hata kuzisuta serikali zao hususan zinapokiuka maandili faafu ya kimaongozi na haki za kibinaadamu.

Kwangu mimi sijaisahau ile historia ya wana Israeli na kwa kweli ina mafunzo mengi kwa viongozi wa sasa wa ki-dini. Imekaririwa bayana katika Biblia Takatifu jinsi wana hawa walivyojipata mateka wa Farao kule Misri na kufanywa watumwa kwa miaka mingi.

Ama kweli jambo hili halikumfurahisha Mungu wetu mwenye Nguvu na pale Mtume Musa hata kama hakuwa wa uzao wa watu Misri, alitumiwa na Mungu kuleta ukombozi wa wana – Israeli.

Hata kama Farao alikuwa na nguvu nyingi na mamlaka kiasi gani ya ki-dunia mwishowe nguvu hizo zake ziliyeyushwa na kudura zake Muumba, na hapa naona kuna funzo makubwa sana kwetu sote na hasa kwa madikteta wote waliosalia katika bara letu la Afrika.

Sikatai najua kwamba mamlaka ya uongozi huwa ni matamu na kwa hakika tumeona yakiwapagawisha marais kadha barani.

Tulikuwa na Idi Amin Dada wa nchi jirani ya Uganda na hata baada ya kuutumia uimla wake kwa wananchi na wapinzani wake, mwisho wake wenye fedheha na majuto ulitimia na hata akafia uhamishoni.

Historia ya ‘mafarao’ wa Afrika ni ndefu, Muammar Gaddafi yu wapi?, Vile vile Saddam Hussein wa Iraq nani hajui mwisho wake alijipata kwenye kitanzi na kuwaacha wananchi wake wajitawale ki-demokrasia?

Orodha ni ndefu, nani angedhani kwamba siku moja rais Al-Bashir wa nchi ya Sudan Kaskazini, angezingirwa na wananchi wake wenye ghadhabu na hatimaye kutimuliwa na wanajeshi wake na kutiwa kizuizini?

Mwenye macho haambiwi tazama, leo hii Afrika kungali na marais wanaotumia kila mbinu kukatalia mamlakani, hawasiti hata kutumia vyombo vya dola kuwakomoa na kuwakomesha wapinzani wao na hata wengine wakizibadilisha katiba za nchi zao ili wabakie mamlakani.

Lakini swali ni je, hali hii itaendelea hadi lini? Hata hivyo najua kwamba Mungu wa Israeli angalipo na halali.

[email protected]